1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kuadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwake

Daniel Gakuba
3 Desemba 2019

Viongozi wa nchi 29 wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanakusanyika mjini London leo katika mkutano wa kilele wa siku mbili ambao unajumuisha pia maadhimisho ya miaka 70 tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo.

Nato-Hauptquartier in Brüssel
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Rais wa Marekani Donald Trump tayari amewasili mjini London kuhudhuria mkutano huo wa kilele, ambao kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kutoka serikali ya Ujerumani, utakuwa muda wa kujitafakari kwa azma ya kuimarisha ushirikiano wa kisiasa miongoni mwa nchi wanachama wa NATO.

Hayo yanaendana na pendekezo la waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas, ambaye ametoa wito wa kujadiliwa kwa matatizo ya ndani ya jumuiya hiyo. Matukio ya hivi karibuni kaskazini mwa Syria yameziacha baadhi ya nchi wanachama katika hali ya mshangao, iliyomfanya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutoa kauli kali, ikiwemo ile kwamba jumuiya ya NATO imekufa kimawazo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia), kaui yake imezua utata. Kushoto ni Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/AP/M. Euler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wengine walijitenga na kauli hiyo ya rais Macron, na kusisitiza kuwa bado jumuiya ya NATO inao umuhimu mkubwa.

Trump anachukua hatua kivyake

Mwezi Oktoba, Marekani iliwaondoa wanajeshi wake kutoka kaskazini mwa Syria katika hali ya kushtukiza, bila kujadiliana kwanza na washirika wengine. Kuondoka kwa vikosi vya Marekani kulitoa mwanya kwa Uturuki ambayo pia ni mwanachama wa NATO, kuwashambulia wanamgambo wa Kikurdi  walikuwa washirika wa nchi za magharibi katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Rais Donald Trump wa Marekani, hatua zake za kushtukiza zinaiweka NATO katika hali tetePicha: picture-alliance/dpa/AP/A. Brandon

Suala jingine linalosababisha misuguano ndani ya NATO, ni shinikizo la mara kwa mara la Rais Donald Trump wa Marekani kwa nchi nyingine wanachama, hususan Ujerumani, akizitaka  kuongeza michango yao, wakati huo huo akitilia mashaka umuhimu wa kipengele muhimu cha mkataba wa jumuiya hiyo, kinachosema kuwa nchi moja ikishambuliwa, imeshambuliwa jumuiya nzima.

Michango zaidi kutoka Ulaya na Canada

Wiki iliyopita katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alitangaza mpango mpya wa michango ya kifedha kwa jumuiya hiyo, akionyesha kuwa nchi tisa wanachama tayari zinachangia angalau asilimia 2 ya pato jumla la ndani katika bajeti ya NATO, na kwamba nchi za Ulaya na Canada zitawekeza kiasi cha dola bilioni 130 katika fuko la jumuiya hiyo, wakati rais Donald Trump akiwa bado madarakani.

Hatua ya Uturuki kununua mfumo wa kujikinga na makombora kutoka Urusi, ni suala jingine litakaloangaziwa sana katika mkutano huu wa NATO wa mjini London.

Pembezoni mwa mkutano huo, mzozo wa Syria utajadiliwa kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

dpae, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW