1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

NATO: Kuisadia Ukraine ni uwekezaji kwa usalama wetu

Hawa Bihoga
15 Februari 2024

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesema kwamba kuchelewesha kupitisha msaada mpya wa Marekani kwa Ukraine, kunavinyongenyeza vikosi vya Ukraine kwenye uwanja wa vita dhidi ya Urusi.

NATO, Ubelgiji | Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pamoja na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pamoja na Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Stoltenberg ameyasema hayo wakati Mawaziri wa Ulinzi kutoka pande zote za muungano wa Nato wakikutana mjini Brussels Ubelgiji kwa mazumzo kuhusiana na masuala ya usalama katikati ya kitisho cha ushindi wa Urusi kwenye vita vyake na Ukraine ambavyo vimedumu kwa takriban miaka miwili sasa.

Mkuu huyo wa NATO amesisitiza juu ya kuendelea kutoa msaada kwa Ukraine na kuutaja uungwaji mkono mpana wa Bunge la Marekani kwa Ukraine.

Amesema kuendelea kuiunga mkono Ukraine kunaleta mabadiliko kwenye uwanja wa vita kila uchao, akitolea mfano siku ya jana ambapo vikosi vya Ukraine vilifanikiwa kushambulia meli ya jeshi la wanamaji wa Urusi.

Akizungumzia uugwaji mkono wa Marekani, amesema anatarajia Washington itafanya uamuzi kwa Bunge na Baraza la Wawakilishi kuendelea kufanikisha msaada kwa Kyiv.

"Ninawashukuru washirika wa NATO wanaotoa msaada,ikiweo mifumo ya ulinzi wa anga," Aliwaambia waandishi wa habari kando na mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi mjini Brussels.

Soma pia:Marekani yapitisha mswada kwa ajili ya Ukraine na Israel

Aliutaja uamuzi wa Umoja wa Ulaya kutenga Euro bilioni 50 kwa Ukraine,ofkutasaidia kueleta tauti kubwa kwa vikosi vya Kyiv katika kupambana na Urusi.

"Na natarajia pia Bunge la Marekani litakubaliana juu ya mfuko wa kuendeleza msaada kwa Ukraine, kwa sababu kusaidia Ukraine si upendo. Kusaidia Ukraine ni uwekezaji katika usalama wetu. Alisisitiza hilo.

Mashambulizi makali yanaendelea Ukraine

Ndani ya Ukraine makabiliano makali yameendelea kushuhudiwa ambapo maafisa wanasema vikosi vya Urusi vimevurumisha makombora 26 dhidi ya Ukraine usiku wa wa kuamkia leo na kuuwa mtu mmoja huku majengo kadhaa ya makaazi yakiharibiwa vibaya. Maafisa hao waliongeza kuwa makombora 13 kati ya hayo 26 yalidunguliwa.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Jeshi la Ukraine limesema limepeleka wanajeshi zaidi katika mji ulioko mashariki mwa Avdiivka unaokabiliwa na mapigano na kuongeza kuwa "hali ni mbaya" katika eneo hilo.

Vikosi vya Urusi vimekuwa vikiuvamia mji huo katika eneo la mashariki la Donetsk tangu mwaka jana na kuuzunguka na pande tatu. Hapo jana Jumatano afisa wa ngazi za juu katika jeshi la Ukraine alikiri kuwa idadi ya wapiganaji ilipungua katika uwanja wa mapambano katika eneo hilo.

Soma pia:Jeshi la Ukraine laizamisha manowari ya Urusi

Vita katika eneo hilo ambalo ni kitovu cha viwanda kaskazini mwa Donetsk vimekuwa na umwagaji damu mkubwa katika kipindi cha miaka miwili ya mapigano, ikilinganishwa na vita katika eneo la Bakhmut ambapo maelfu ya wanajeshi waliuwawa.

Tangu kuzuka kwa vita takriban miaka miwili iliopita vikosi vya Urusi vimeshambulia kwa kiasi kikubwa miundombinu muhimu nchini Ukraine na kusababisha hali ya maisha kwa wakaazi kuwa tete.

Katika utafiti mpya uliofanywa na Benk ya Dunia, Umoja wa Mataifa, Tume ya Ulaya na serikali ya Ukraine uligundua kwamba kujenga upya uchumi wa taifa hilo kutagharimu dola bilioni 486, ikiwa ni mara mbili zaidi ya pato lake la kiuchumi lililotarajiwa mnamo 2023.

Ripoti hiyo ilisema uharibifu wa moja kwa moja kutokana na vita ulikuwa umefikia karibu dola bilioni 152, na hasara zilijilimbikizia katika mikoa kama Donetsk, Kharkiv, Luhansk, Zaporizhzhia, Kherson na Kyiv.

Usumbufu wa pato la kiuchumi na biashara, pamoja na gharama zingine zinazohusiana na vita, kunaweza kuongeza dola bilioni 499.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW