NATO, Urusi wafanya luteka mkabala bahari ya Baltiki
14 Juni 2019
Luteka hizo za kijeshi za umoja wa kujihami wa NATO zilizopachikwa jina la Baltops 2019, zilianza tarehe 9 mwezi huu wa Juni na zitaendelea hadi tarehe 21. Mazoezi ya aina hiyo yamefanyika katika bahari hiyo kwa muda wa miaka 40 iliyopita, lakini tangu Urusi ilipoinyakua rasi ya Crimea kutoka Ukraine, NATO imejiimarisha kwenye mpaka wake wa Mashariki.
Mnamo miaka ya hivi karibuni vimetokea visa kadhaa ambapo ndege za NATO ziliingilia kati kuzizuia ndege za kivita za Urusi kuingia katika anga la nchi wanachama wa muungano huo wa kijeshi.Kikosi kilichovuma enzi za vita baridi charejeazifanya luteka za NATO za mwaka huu kuwa za aina ya kiepekee ni kwamba zinaongozwa na kikosi cha pili cha jeshi la majini la Marekani, ambacho enzi za vita baridi kilipata umaarufu kwa kushiriki katika operesheni kadhaa za kimkakati, ikiwemo ya kukizingira kisiwa cha Cuba wakati wa mzozo wa makombora baina ya Marekani na iliyokuwa Umoja wa Kisovieti.
Kikosi kilichovuma enzi za vita baridi charejea
Kikosi hicho kiliwahi kuvunjwa mwaka 2011, kwa sababu uongozi wa rais Barack Obama uliamini kwamba Urusi haikuwa kitisho tena kwa nchi za Magharibi, lakini kilirejeshwa mwaka 2018 baada ya Urusi kuimarisha shughuli zake katika bahari ya Atlantiki.
Lakini mkuu wa kikosi hicho Andrew Lewis ameiambia DW kwamba kurejeshwa kwa kikosi chake hakuilengi nchi yoyote, bali ni jibu kwa mazingira ya kiusalama yanayobadilika duniani, kutokana na kuibuka kwa washindani wapya kijeshi, hasa Urusi na China.
Luteka za Baltops 2019 zinahusisha wanajeshi 8,600 kutoka nchi 16, na nchi mbili za ukanda wa Baltiki, Sweden na Finland ambazo sio wanachama. Wanatumia manowari 50, nyambizi mbili na ndege za kivita zipatazo 40. Mazoezi yao yanajikita katika ulinzi wa anga na kujilinda dhidi ya manowari za adui.
Urusi yakaa chonjo
Kwa urusi, luteka hizi zinazofanyika katika jamhuri tatu za Baltiki za Estonia, Latvia na Lithuania ambazo zilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti lakini sasa ni wanachama wa NATO, zinatazamwa kwa jicho la wasiwasi.
Wakati wanajeshi wa NATO wakijizoeza kuwasili kwa meli kwenye fukwe za kisiwa cha Estonia cha Saaremaa, wale wa Urusi wanafanya luteka zao katika bahari hiyo hiyo, wakijizoeza kuzizamisha nyambizi za adui, na kuzilenga meli zake kwa makombora kutoka eneo inalolithibiti la Kaliningrad.
dw - https://p.dw.com/p/3KOGx