1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO: Urusi yapeleka wanajeshi zaidi mpakani

16 Februari 2022

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeituhumu Urusi leo kwa kuwaongeza wanajeshi zaidi kwenye mpaka wa Ukraine, hata wakati Moscow ilisema inawaondoa askari wake na kuwa ipo tayari kwa diplomasia.

Russland I BMP-3 Infanterie
Picha: Sergey Pivovarov/Sputnik/dpa/picture alliance

Wakati akiufungua mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa NATO mjini Brussels, Katibu Mkuu Jens Stoltenberg alionekana kutoshawishika kuwa kitisho cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kimepungua, na akaelezea matumaini finyu ya kuwepo suluhisho la diplomasia. "Tunachokiona ni kuwa wameongeza idadi ya wanajeshi, na wanajeshi zaidi wako njiani kuelekea huko. kwa hiyo mpaka sasa, mzozo haujatulizwa. Lakini bila shaka pia tunausikia ujumbe wa pande zote kuhusu diplomasia na tuko tayari kushiriki katika juhudi za kidiplomasia na Urusi."

Soma pia: NATO yatilia mashaka uondoaji zaidi wa askari wa Urusi

Moscow inataka kulizuia taifa hilo lililokuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO. NATO imekataa kukubali takwa hilo na mawaziri wa ulinzi wanakutana leo kuonyesha msimamo wa pamoja.

Urusi imesema inawaondoa wanajeshi mpakani UkrainePicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Urusi imechapisha video ambayo ilisema inaonyesha msafara wa vifaru, magari ya kivita na vikosi vya kijeshi ukiondoka rasi ya Crimea ambayo Moscow iliinyakua mwaka wa 2014.

Stoltenberg ametahadharisha kuwa Urusi mara kwa mara huvihamisha vifaa vya kijeshi na askari wake mpakani hapo. Na kwa kufanya hivyo, haimaanishi kuwa wanawaondoa wanajeshi wake.

NATO inatafakari hatua mpya za kuiwekea kizuizi Urusi kwenye mpaka wake wa mashariki, kama jibu kwa kitisho cha Urusi katika upande wa kaskazini mwa Ukraine, mashariki na kusini. Wanadiplomasia wamesmea huenda ikahusisha wanajeshi wapya 4,000 katika vikundi vinne vya mapambano nchini Romania, Bulgaria na huenda pia Hungary na Slovakia.

Mawaziri wa ulinzi pia wanazingatia hatua za muungano huo za kukabiliana na zana za nyuklia ijapokuwa mazungumzo ni ya faragha. Urusi imekusanya kiasi kikubwa cha zana za nyuklia.

Marekani imewapeleka wanajeshi Poland na RomaniaPicha: Reuters

Watajadili vipi na lini wanapaswa kupeleka kwa dharura wanajeshi na vifaa katika nchi zilizoko karibu na Urusi na ukanda wa Bahari Nyeusi ikiwa Moscow itaamuru uvamizi wa Ukraine.

Marekani imeanza kupeleka wanajeshi 5,000 nchini Poland na Romania. Uingereza inatuma mamia ya wanajeshi nchini Poland na kutoa manowari zaidi na ndege. Ujerumani, Uholanzi na Norway zinatuma wanajeshi wa ziada nchini Lithuania. Denmark na Uhispania pia zinatoa ndege za kivita kwa ajili ya doria za angani.

Wakati huo huo, Ukraine imefanya leo mazoezi ya kijeshi na maonyesho mengine ikiwemo kupeperusha bendera ya taifa kudhihirisha uzalendo na umoja.

Soma pia: Urusi yaongezewa shinikizo la kuondoa wanajeshi wake

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwatizama wanajeshi wakipewa mafunzo kwa kutumia baadhi ya zana mpya ilizopewa na nchi za magharibi za kuvilipua vifaru, katika eneo karibu na Rivne, magharibi ya mji mkuu Kiev. Hayo yalifanywa wakati mamia ya raia wakiandamana kwa amani hadi katika uwanja wa michezo mjini Kiev kuonyesha mshikamano.

afp, ap, dpa, reuters

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi