1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwezekano wa kufikiwa makubaliano na Urusi ni mdogo

10 Januari 2022

Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi wamefanya mazungumzo muhimu katika juhudi za kidiplomasia za hivi karibuni zinazolenga pamoja na mengine kumaliza mvutano kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya juu ya Ukraine.

Belgien I Jens Stoltenberg I NATO
Picha: Johanna Geron /REUTERS

Hata hivyo hakuna matumaini makubwa ya kupatikana kwa muafaka kuhusu mgogoro huo. 

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov na ujumbe wake waliwasili katika ubalozi wa marekani mjini Geneva kwa mazungumzo ya ana kwa ana pamoja na naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman na kikosi chake.

soma Mawaziri wa NATO wakutana kujadili msimamo wa pamoja kwa Urusi

Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA Novosti, limemnukuu Ryabkov akisema anahofia kuwa Washington haichukulii kwa uzito ombi la Moscow la kusitisha upanuzi wa jumuiya ya kujihami ya NATO kuelekea mashariki.

Sherman kupitia mtandao wa Twitter aliandika kuwa mazungumzo yanaendelea lakini kutakuwa na maendeleo madogo bila ya kuwepo kwa washirika wake hasa linapokuja suala la usalama wa Ulaya.

Muafaka utapatikana?

Wendy Sherman na Sergej RjabkowPicha: Denis Balibouse/KEYSTONE/REUTERS/dpa/picture alliance

Pande zote mbili zimeweka msimamo thabiti, huku Marekani ikionya kwamba Urusi itakabiliwa na athari kubwa za kidiplomasia na kiuchumi ikiwa itaivamia Ukraine, na Urusi ikitaka kuwepo kwa mipango mipya ya kiusalama na nchi za Magharibi.

Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO amesema "Sidhani tunaweza kutarajia mikutano hii itasuluhisha mambo yote, tunachotarajia ni kukubaliana juu ya njia ya mbele. Ili tukubaliane mfululizo wa vikao, tukubaliane juu ya mchakato." Kwa hivyo sio kweli kutarajia kwamba tukimaliza wiki hii, tukimaliza mikutano ambayo imepangwa kwamba  shida itatatuliwa."

soma Marekani yasema itaijibu Urusi iwapo itaivamia Ukraine

 Uchokozi wa Urusi 

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Andrew Harnik/AP/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken siku ya Jumapili alisisitiza kwamba Urusi inapaswa kuchagua kati ya mazungumzo ua makabiliano, na matokeo chanya kutoka kwa mazungumzo yatategemea iwapo Urusi ina nia kusitisha uchokozi, ambao aliutaja kama "mazingira ya kuongezeka kwa bunduki zinazokilenga kichwa cha Ukraine".

Jumatano utafanyika mkutano mwingine baina ya jumuiya ya kujihami ya NATO na Urusi mjini Brussels, kisha baraza la kudumu la Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) litakutana mjini Vienna siku ya Alhamisi huku suala la Ukraine likitarajiwa kutawala mkutano huo.

soma Putin, Biden wazungumzia mzozo wa Ukraine

Mkutano huo ni sehemu ya majadiliano ya kimkakati ya usalama yaliyoanzishwa na rais Joe Biden pamoja na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mnamo mwezi Juni mwaka jana.

 

AFP/DPA