1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

NATO yadokeza kuipa Ukraine zana za nguvu zaidi

16 Januari 2023

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema Ukraine itarajie silaha zaidi nzito nzito hivi karibuni.

Litauen Camp Adrian Rohn 2022 | Leopard 2-Panzer der Bundeswehr
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeahidi kuipa Ukraine silaha nzitonzito zaidi hivi karibuni. Ahadi hiyo imejiri siku moja tu baada ya zaidi ya watu 30 kuuawa Ukraine kufuatia mashambulizi ya Urusi, huku Rais Vladimir Putin akivipongeza vikosi vyake vilivyodai kuukamata mji wa Soledar.

Huku idadi ya vifo ikipindukia 30 na shughuli za kufukua vifusi na kutafuta makumi ya watu ambao bado hawajulikani waliko ikiendelea, baada ya Urusi kushambulia kwa kombora jengo la ghorofa la makaazi ya watu siku ya Jumamosi, katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema Ukraine itarajie silaha zaidi nzito nzito hivi karibuni kutoka kwa washirika wake. Hiyo ni kufuatia ombi la Ukraine kwa washirika wake kuipa vifaru, makombora na zana zaidi ambazo ni muhimu katika kujilinda.

NATO, EU zaapa uungaji mkono zaidi kwa Ukraine

Stoltenberg ameliambia jarida la kila siku la Ujerumani Handesblatt kwamba ahadi za hivi karibuni za kuipa Ukraine zana nzitonzito ni muhimu na anatarajia ahadi zaidi zitatolewa siku zijazo. Amesema hayo kuelekea mkutano utakaofanyika wiki hii, wa kundi linaloratibu shughuli za usambazaji silaha kwa Ukraine.

KAtibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens StoltenbergPicha: Johanna Geron/REUTERS

Shughuli za kutafuta manusura au miili yaendelea Dnipiro

Shambulizi hilo la Urusi siku ya Jumamosi limelaaniwa vikali na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

"Kwa sasa hatima ya zaidi ya watu 30 ambao huenda walikuwa kwenye jengo hilo lililoko Dnipro wakati kombora la magaidi liliposhambulia haijulikani. Makumi ya watu waliokolewa, wakiwemo Watoto sita. Tunapambana kumpata kila mtu," amesema Zelensky.

Mnamo Jumamosi, Rais Zelensky aliziomba nchi za magharibi silaha zenye nguvu zaidi, akisema 'ugaidi' wa Urusi unaweza kukomeshwa tu katika uwanja wa mapambano.

NATO na EU kushirikiana zaidi kufuatia uvamizi wa Ukraine

Mapema mwezi huu, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ziliahidi kuipa Ukraine, vifaru magari maalum ya kivita miongoni mwa silaha nyingine.

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: President of Ukraine/apaimages/IMAGO

Lakini kuna ongezeko la shinikizo kwa washirika wa Ukraine kupiga hatua zaidi na wakubaliane kuipa Ukraine silaha zenye nguvu na ubora zaidi.

Uingereza yaahidi vifaru 14

Mnamo Jumamosi, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliahidi kuipa Kiev vifaru 14 aina ya Challenger 2.

Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza ilitahadharisha kuwa kupeleka vifaru hivyo katika uwanja wa mapambano, kutachochea mashambulizi zaidi, na maafa mengi hata kwa raia.

Siku chache tu baada ya Urusi kudai kuukamata mji wa Soledar ulioko mashariki mwa Ukraine. Rais Putin amepongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa ufanisi mkubwa.

Mji huo mdogo uliokuwa na wakaazi 10,000 kabla ya uvamizi, unaweza kuwa muhimu kwa vikosi vya Urusi katika juhudi zao za kutaka kuukamata mji wa kimkakati wa Bakhmut ambao umekuwa lengo lao kuu tangu mwezi Oktoba.

(Chanzo: AFPE) (Mwandishi: John Juma)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW