1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yahitaji mkakati mpya karne ya 21

N.Werkhäuser - (P.Martin)12 Novemba 2008

Kwa maoni ya serikali ya Ujerumani,uimarishaji wa Afghanistan ni kipaumbele cha Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi NATO.Lakini shirika hilo pia linahitaji mkakati mpya kutekeleza wajibu wake katika karne ya 21.

Kuimarisha usalama na utulivu nchini Afghanistan bado ni tatizo kubwa la serikali ya Ujerumani katika siasa zake za nje.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipohotubia mkutano wa kila mwaka wa German Atlantic Society mjini Berlin alisisitiza jinsi ilivyo muhimu kwa NATO kutimiza ujumbe wake nchini Afghanistan.Hadhi ya shirika hilo amesema,inategemea mafanikio yatakayopatikana huko Afghanistan.Vikosi vya Ujerumani vya wanajeshi 4,500 vitabakia Afghanistan mpaka utulivu na usalama utakapopatikana nchini humo.Lakini anaitaraji serikali ya Afghanistan pia kuwajibika zaidi katika siku zijazo na kuwa na msimamo wazi wazi kupiga vita madawa ya kulevya.Kwa maoni yake ushirikiano kati ya majeshi na wasaidizi wa kiraia ni utaratibu wa usalama utakaoweza kufanya kazi nchini Afghanistan.

Merkel hakusita kueleza msimamo wa serikali yake kuhusu uwezekano wa kuombwa na Marekani mwakani kupeleka wanajeshi zaidi nchini Afghanistan. Amesema,Berlin ipo tayari kupeleka ndege zingine za upelelezi aina ya AWACS,lakini mwaka 2009 haina mpango wa kupeleka wanajeshi zaidi.Mada ya ujumbe huo inazusha mabishano nchini Ujerumani.

Na alipogeukia suala la Urusi,Merkel alisema ushirikiano kati ya nchi wanachama wa NATO kamwe hauwezi kuvunjwa.Hata katika mazungumzo yake na washirika wa Kirusi,mara kwa mara amewaambia kuwa jeribio hilo limeshindwa tangu miongo kadhaa na hata katika siku zijazo halitofanikiwa.

Hata hivyo Merkel alisisitiza kuwa Urusi ni mshirika muhimu wa Ujerumani. Ni dhahiri kuwa NATO itaendelea kushughulishwa na suala la Georgia na hata Ukraine inayotaka kuwa mwanachama katika shirika hilo la kujihami. Merkel amesema,nchi zote mbili zinaweza kuwa wanachama wa NATO ikiwa zinataka kufanya hivyo na iwapo washirika wa NATO wanakubali. Lakini yeye haamini kuwa nchi hizo zitaweza kutimiza masharti ya uanachama,hali halisi inayokutikana katika nchi hizo ikizingatiwa. Amesema,kilicho muhimu zaidi kwenye mkutano ujao wa viongozi wa NATO ni kuwasilisha mpango wa mkakati mpya utakaoeleza wazi wazi wajibu wa shirika hilo katika karne ya 21.