NATO yashambulia Tripoli
10 Mei 2011Mashambulio ya jeshi la NATO yameutikisa mji wa Tripoli wakati waasi katika mji uliozingirwa wa Misrata wamesema kuwa wanayasukuma majeshi ya Muammar Gaddafi nyuma na umoja wa mataifa unaonya kuwa Libya inaathirika kutokana na upungufu mkubwa wa bidhaa na huduma.
Ndege za kijeshi zilikuwa zikipita chini chini katika mji mkuu wa Libya Tripoli mapema leo asubuhi, zilishambulia kwa mabomu kwa muda wa saa tatu hivi, ameeleza mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP. Jana Jumatatu watu walioshuhudia wamesema kuwa kulikuwa na miripuko miwili katika mji huo mkuu, na kuongeza kuwa moshi ulikuwa ukitoka kutoka katika eneo karibu na ofisi za kituo cha televisheni ya Libya na shirika la habari la nchi hiyo JANA.
Miripuko hiyo imetokea baada ya katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen kusema kuwa muda unaelekea mwisho kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, ambaye anapaswa kutambua haraka kuwa hana muda tena katika uongozi wake ama serikali yake.
Maafisa wa Libya wamesema kuwa watoto wanne wamejeruhiwa, wawili kati yao vibaya sana, kutokana na vipande vya chupa kutoka katika madirisha baada ya nyumba kushambuliwa kwa mabomu ya NATO. Maafisa wamewaonyesha waandishi habari kutoka nje hospitali katika mji mkuu Tripoli ambako madirisha yameharibiwa, kutokana na mashambulio hayo , ambayo yameharibu mnara wa mawasiliano ulipo karibu na hospitali hiyo.
Msemaji wa serikali Mussa Ibrahim amesema kuwa mashambulio hayo ya NATO hayavumiliki.
Hii ni operesheni ya wazi ya kutaka kumuua kiongozi wa nchi hii. Hali hii haikubaliki katika sheria za kimataifa.
Waandishi wa habari pia wamepelekwa kuona jengo la serikali ambalo ipo taasisi ya kuwahudumia watoto ambalo limeharibiwa kabisa. Jengo hilo la kizamani lililojengwa na wakoloni limeharibiwa kutokana na mashambulio ya NATO ya Aprili 30.
Hakuna taarifa zaidi zilizopatikana, lakini miripuko mjini Tripoli imetokea huku kukiwa na mkwamo katika vita hivyo vya waasi kutaka kumuondoa kanali Muammar Gaddafi madarakani pamoja na kutokea mkanganyiko kwa mataifa ya magharibi kuhusu iwapo yatoe msaada kwa waasi. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuwa mashambulio hayo hayamlengi mtu.
Mashambulio haya yanalenga kushambulia maeneo ya kijeshi na sio watu binafsi. Na sera hii imefuatwa kwa utaratibu maalum.
Mzozo huo, kuharibika kwa mifumo ya kutawala serikalini na upungufu wa fedha na mafuta unasababisha matatizo makubwa kwa wananchi wa kawaida nchini Libya, Valerie Amos, mratibu wa masuala ya kiutu wa umoja wa mataifa , ameliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa. Upungufu mkubwa wa bidhaa na huduma unaathiri nchi hiyo kwa njia mbazo zitaathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wa kawaida.
Baada ya mashambulio makali , waasi sasa wanadhibiti eneo la pwani magharibi ya mji wa Misrata, mji wa tatu kwa ukubwa , ambao majeshi ya Gaddafi yanaushambulia kwa zaidi ya miezi miwili na kusababisha maelfu ya watu kuukimbia. Kwa jumla umoja wa mataifa umesema jana kuwa karibu watu 750,000 wameikimbia Libya tangu majeshi ya Gaddafi kuanza kuwashambulia waandamanaji wanaoipinga serikali.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre/
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman