NATO yasita kuikabili Urusi licha ya shinikizo la washirika
25 Septemba 2025
Mataifa yaliyo kwenye mpaka wa mashariki wa NATO yanahisi tishio la moja kwa moja kutoka Moscow na ndiyo yaliyo mstari wa mbele kudai msimamo mkali.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk alisema Warsaw itachukua hatua kali dhidi ya ukiukaji wowote wa anga yake. Wakati huo huo, waziri wake wa mambo ya nje, Radoslaw Sikorski, aliionya Urusi "kutolalamika” iwapo ndege zake zitaangushwa.
Waziri wa Ulinzi wa Lithuania, Dovile Sakaliene, alikumbusha kuwa miaka 10 iliyopita Uturuki iliangusha ndege ya kivita ya Urusi iliyoingia kutoka Syria, tukio lililosababisha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia kati ya Ankara na Moscow. Rais wa Marekani Donald Trump pia aliongeza shinikizo akisema wazi kuwa ndege za Urusi zikikiuka anga la NATO "zinapaswa kushushwa chini.”
Lakini si wote wanaopigia debe njia ya risasi. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliwaonya washirika wasiangukie "mtego wa kuchochea mgogoro.” Alisema matamshi ya pupa ya kuonyesha nguvu hayasaidii wakati huu. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron naye alisema NATO inapaswa "kuongeza hatua” zake, lakini akasisitiza: "Hatutafungua moto.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alitoa kauli isiyoendana na rais wake, akisema hakuna mjadala wa moja kwa moja wa kudungua ndege za Urusi "isipokuwa ziwe zinashambulia.”
Msimamo wa NATO
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte amesema wazi kuwa jumuiya hiyo itachukua hatua tu endapo ndege itahesabiwa kuwa tishio. "Tuko tayari kulinda miji yetu, watu wetu na miundombinu yetu,” alisema, lakini akasisitiza kuwa hilo halimaanishi kila mara ndege itapigwa chini mara moja.
Mfano uliojitokeza hivi karibuni ni wakati droni 20 za Urusi zilipoingia anga ya Poland na baadhi kudunguguliwa na NATO kwa sababu zilitazamwa kama hatari. Hilo lilikuwa tukio la kwanza la NATO kudungua ndege za Urusi tangu uvamizi wa Ukraine mwaka 2022. Lakini ilipokuwa Estonia, ndege tatu za kivita za Urusi ziliingia kwa dakika 12 pekee na NATO ilizisindikiza bila kuchochea zaidi.
Msimamo wa NATO ni mmoja, lakini kila mwanachama anaweza kuwa na kanuni tofauti za kukabiliana na ukiukaji wa anga. Poland au nchi nyingine zinaweza kuchukua hatua kivyao, lakini mara nyingi zinategemea washirika wao kwa ulinzi wa anga. Estonia kwa mfano haina ndege zake za kivita na hivyo hutegemea msaada wa wanachama wengine.
Kuzidisha ulinzi mashariki
Badala ya kubadili kanuni, NATO inalenga kuimarisha ulinzi wake kwenye mpaka wa mashariki. Baada ya tukio la Poland, ilizindua operesheni mpya iitwayo Eastern Sentry huku mataifa kadhaa yakipeleka ndege zao nchini humo.
Hata hivyo, wanadiplomasia wa jumuiya hiyo wanasema bado kuna mapungufu, hasa katika silaha za bei nafuu zinazoweza kushughulikia mashambulizi ya droni kwa ufanisi zaidi – silaha ambazo Ukraine imekuwa ikizitumia.
Umoja wa Ulaya kwa upande wake umetangaza mpango wa kuunda "ukuta wa droni” kufuatilia ukiukaji wa anga, ingawa bado maelezo ya utekelezaji wake hayajatolewa.
Pamoja na tofauti za matamshi ya viongozi wake, NATO imesisitiza kuwa mstari wake ni wazi – haitafungua moto isipokuwa pale ambapo ndege inachukuliwa kama tishio la moja kwa moja. Wakati huo huo, mashariki mwa Ulaya, woga wa mzozo kusambaa unazidi kuimarisha miito ya hatua kali.