1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yatafakari kusaidia juhudi za amani ukanda wa Sahel-UN

Daniel Gakuba
8 Oktoba 2021

Jumuiya ya kujihami ya NATO inachunguza uwezekano wa kupeleka msaada wa kuunga mkono operesheni dhidi ya wapiganaji wa jihadi katika ukanda wa Sahel. Hayo ni kulingana na barua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mali Sahelzone l Anti-Terror-Operation Barkhane in der afrikanischen Sahelzone im Norden Malis, Marcon
Ndege za kijeshi za Ufaransa, nchi mojawapo inayounga mkono operesheni dhidi ya wanajihadi katika Ukanda wa SahelPicha: Christophe Petit Tesson/abaca/picture alliance

Azma hiyo ya Jumuiya hiyo ya kujihami ya nchi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini imeainishwa katika barua ya Katibu Mkuu wa Mataifa Antonio Guterres ambayo shirika la habari la AFP limeona nakala yake. Msaada huo wa NATO unanuiwa kuvipiga jeki vikosi vya nchi tano katika muungano ujulikanao kama G5, katika eneo la mpaka kati ya Mali, Niger na Burkina Faso.

Soma zaidi: Vikosi vya Ufaransa vyamuuwa mkuu wa IS ukanda wa Sahel

Barua ya Katibu Mkuu Guterres kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Matifa ilisema uungaji mkono huo wa NATO utapitia kitengo cha Msaada na Vifaa. Amesema katika barua hiyo kuwa amejiridhisha na kuwepo haja ya kuanzishwa ofisi ya usaidizi ya Umoja wa Mataifa kwa vikosi vya G5, ambavyo vinashirikisha wanajeshi wapatao 5,000 kutoka Mali, Mauritania, Niger, Chad na Burkina Faso, akitumai ofisi hiyo itafadhiliwa kifedha na Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: John Minchillo/POOL/AP/picture alliance

Mpango wa namna hiyo, amesema Guterres, unaweza kuwa wenye tija zaidi katika kutoa msaada wa kuaminika na kutabirika kwa vikosi hivyo vya pamoja.

Marekani yasitasita kuupitisha msaada wake katika Umoja wa Mataifa

Hata hivyo, Marekani ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa katika bajeti ya Umoja wa Mataifa, imeukataa mpango huo, unaopigiwa debe na Ufaransa na mataifa kadhaa ya kiafrika.

Soma zaidi: Wanajeshi 15 wa Kijerumani wajeruhiwa Mali

Mwezi Juni, naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Jeffrey DeLaurentis alisema nchi yake inataka juhudi za kupigana na ugaidi ziendelee kutenganishwa na zile za kuhifadhi amani, kwa lengo la kulinda hadhi ya Umoja wa Mataifa kama taasisi isiyoegemea upande wowote.

Nchi tano za Ukanda wa Sahel zinashiriki katika Kikosi cha G5Picha: Getty Images/AFP/M. Cattani

Kwa miaka mingi Marekani imekuwa ikisema inapendelea kutoa msaada wake kwa nchi za ukanda wa Sahel moja kwa moja badala ya kupitia Umoja wa Mataifa.

Makubaliano kuhusu msaada, tofauti katika kuufikisha

Katibu Mkuu Guterres amesema kuundwa kwa ushirika wa kijeshi wa G5, licha ya changamoto lukuki zilizopo, ni ishara yenye nguvu ya utashi wa kisiasa wa nchi tano husika, ambayo inahitaji kuungwa mkono kikamilifu na jumuiya ya kimataifa.

Soma zaidi: Guterres alaani mauaji ya watu 160 nchini Burkina Faso

Ameongeza kuwa ingawa pande zote zinazochangia mawazo zinaunga mkono msaada kwa vikosi vya G5 kama juhudi ya kipekee inayostahili kuungwa mkono kimataifa, hakuna muafaka juu ya njia bora ya kuufikisha msaada huo.

Ghasia za wanamgambo zimeangamiza mali na maisha Ukanda wa SahelPicha: Getty Images/AFP/M. Cattani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya rais wake wa sasa ambaye ni Kenya, linapanga kupeleka ujumbe nchini Mali na Niger mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, kwa lengo la kubaini hali halisi ya kiusalama.

Guterres amesema kuwa Umoja wa Afrika umedhihirisha utayari wake wa kuratibu ushirikiano wa kiusalama katika Ukanda wa Sahel, huku lakini ukisisitiza kuwa utahitaji msaada wa kifedha kuweza kugharimia mahitaji ya kivifaa.

Kwa wakati huu Umoja wa Mataifa unasaidia vikosi vya G5 kwa kuvipa mafuta, maji na chakula, kupitia ujumbe wake wa kulinda amani nchini Mali, Minusma na pia msaada wa kimatibabu kupitia ufadhili mwingine.

 

afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW