NATO yazindua kikosi kipya cha kuweka doria Bahari ya Baltic
14 Januari 2025Hayo yameelezwa Jumanne na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte katika mkutano wa kilele wa nchi za eneo la Baltic, ambazo ni wanachama wa NATO, ambao unajadili usalama katika ukanda huo. Nyaya kadhaa za mawasiliano ya simu, umeme na intaneti chini ya bahari zilikatwa katika eneo hilo, huku wataalamu na wanasiasa wakiishutumu Urusi kwa kuchochea mvutano dhidi ya mataifa ya Magharibi, huku pande hizo mbili zikizozana kuhusu vita vya Ukraine.
Lengo kuu la mkutano huo unaofanyika Helsinki, Finland, ni kutafuta njia za kuilinda vyema miundombinu muhimu katika Bahari ya Baltic na kukabiliana na kitisho cha kile kinachoitwa ''meli za kivuli'' za mafuta za Urusi ambazo husafiri kwa siri. Hilo linazihusisha meli ambazo Urusi inazitumia kusafirisha mfano mafuta, ili kukwepa vikwazo vilivyowekwa kutokana na uvamizi wake wa Ukraine.
NATO yajizuia kumpa faida adui
Rutte amesema ujumbe huo unaojulikana kama ''Baltic Sentry'' utajumuisha vifaa mbalimbali, ikiwemo manowari zaidi, droni za majini, satelaiti na ndege za kivita zinazofanya doria baharini. Hata hivyo, amesema hawezi kuelezea idadi ya meli zitakazotumika, kwa sababu inaweza kutofautiana kutoka wiki moja hadi nyingine, na pia NATO haitaki kueleza kila kitu mbele ya adui yake.
''Tumekubaliana leo kuzindua mpango wa kupeleka teknolojia mpya kwa juhudi hii, ikiwemo droni za baharini ili kulinda, na kuzuia kitisho. Pia tunashirikiana na washirika wetu kuunganisha juhudi zao za kiulinzi na NATO, ili kuhakikisha kuwa tunagundua kikamilifu kitisho,'' alithibitisha Rutte.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema jeshi la wanamaji la nchi yake litachangia meli ili kuilinda miundombinu katika Bahari ya Baltic. Scholz ameyasema hayo Jumanne wakati akihudhuria mkutano wa usalama katika Bahari ya Baltic. Kulingana na Scholz, Ujerumani ilikuwa tayari kuchukua jukumu kwa kutumia rasilimali zake kwa kuzingatia kitisho kinachoongezeka.
Huku hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov Jumanne ameishutumu Marekani kwa kujaribu kuvuruga bomba la kusambazia gesi la TurkStream kwenda Ulaya, kwa msaada wa mashambulizi ya droni ya Ukraine. Lavrov amesema Marekani inahamasisha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya miundombinu ya nishati ya nchi yake, na amedai kuwa kuna mipango ya kulilenga bomba la TurkStream. Kulingana na Lavrov, Marekani inataka kusambaratishwa kwa bomba la TurkStream, kufuatia hujuma zilizofanywa kwenye bomba la gesi la Nord Stream.
Zelensky afanya mazungumzo na Macron
Ama kwa upande mwingine, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema kwamba amefanya mazungumzo zaidi na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kuhusu uwezekano wa kupelekwa majeshi ya nchi za Magharibi nchini Ukraine ili kulinda mpango wowote wa amani wa kumaliza vita na Urusi vilivyodumu kwa takribani miaka mitatu. Zelansky ameyatoa matamshi hayo kabla ya ziara rasmi ya Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius mjini Kiev.
Pistorius amewasili Jumanne mjini Kiev kwa ziara ambayo haikutangazwa awali, siku moja baada ya mkutano na mawaziri wenzake wa Poland, Ufaransa, Uingereza na Italia, uliofanyika mjini Warsaw, kujadiliana kuhusu kupeleka silaha kwa Ukraine.
(AFP, DPA, AP, Reuters)