1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Navalny amkejeli Putin, ''Mfalme yuko uchi''

Angela Mdungu
29 Aprili 2021

Alexei Navalny, mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi amemkejeli Rais Vladmir Putin akimfananisha na "mfalme" aliye uchi wakati kesi yake iliposikilizwa leo Alhamisi 29.04.2021.

Russland Oppositionsführer Alexej Nawalny
Picha: VASILY MAXIMOV/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa chaneli huru ya mtandaoni ya Dohzd, Navalny ameonekana akiyasema hayo katika video kutoka mahakamani. Katika video hiyo, Navalny ambaye ameonekana kwa mara ya kwanza tangu alipositisha mgomo wa chakula kando ya maneno hao ya kejeli amesema kuwa ikiwa Putin ataendelea kutawala, muongo mmoja ulioibiwa utaongezwa katika muongo mwingine ambao umekwishakupotea.

"Ningependa kusema kwako mpendwa mahakama, mfalme wako yuko uchi, na zaidi ya mvulana mmoja mdogo anapiga kelele kuhusu hilo, tayari mamilioni ya watu wanapaza sauti juu ya hili. Miaka 20 ya kushindwa kuongoza imesababisha matokeo yafuatayo; kofia yake ya kifalme inaangukia masikioni mwake, kuna uongo mwingi kwenye televisheni, tumetumia fedha nyingi na nchi yetu inaendelea kudidimia kwenye umasikini. Katika hali isiyo ya kushangaza wachumi wanaandika barua na kusema miaka michache iliyopita inapaswa kuitwa muongo uliopotea.'' alisema Navalny.

Kesi ya leo ya Navalny ilihusu jaribio la kutaka kupinga hukumu na faini alizotozwa mwezi Februari kwa tuhuma za kumchafua mkongwe wa Vita ya Pili ya Dunia. Kama ilivyotarajiwa, mahakama iliamua kushikilia uamuzi wake hii ikimaanisha kuwa ni lazima Navalny alipe faini ambayo ni sawa na dola 11,400 za Kimarekani ambazo ni mara mbili ya mshahara wa mwaka mzima wa mfanyakazi mwenye kipato cha wastani nchini Urusi.

Wanasheria  wake kuipeleka kesi mahakama ya Ulaya ya haki za binadamu

Wanasheria wake wametangaza kuwa wataipeleka kesi ya mkosoaji huyo wa Rais Putin kwenye mahakama ya Ulaya ya haki za Binadamu. Navalny, mwenye umri wa miaka 44, alihudhuria kesi hiyo kwa njia ya video akiwa katika gereza anakoshikiliwa kwa karibu siku mia moja sasa. Wiki iliyopita, alisitisha mgomo wake wa kula wiki kadhaa baada ya ushauri wa madaktari wake waliohofia usalama wa maisha yake.

Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Alexei Druzhinin/AP/picture alliance

Mpinzani huyo wa Putin aliyeponea chupuchupu jaribio la kuuwawa kwa sumu mwaka uliopita, amekuwa akikabiliwa na kesi kadhaa tangu alipokamatwa Urusi akitokea Ujerumani mnamo mwezi Januari.

Katika hatua nyingine, mmoja wa wafanyakazi wa juu wa Navalny amesema timu za siasa za mwanasiasa huyo zitasitisha shughuli zake kutokana na hatua ya mahakama ya hivi karibuni. Washirika wake wanasema anakabiliwa na tuhuma mpya na kwamba wamelazimika kufunga ofisi za kikanda za mtandao wa kampeni zake ambazo serikali inataka kuzipiga marufuku kwa kuwa na msimamo mkali.