1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Navalny kukata rufaa dhidi ya kifungo cha jela

Yusra Buwayhid
3 Februari 2021

Wanasheria wa kiongozi wa upinzani Urusi, Alexei Navalny, wamesema watakata rufaa kupinga adhabu ya kifungo cha miaka mitatu na nusu jela aliyohukumiwa mpinzani huyo.

Russland Alexej Nawalny vor Gericht in Moskau
Picha: Press service of Moscow City Court/Reuters

Mahakama imesema Navalny alivunja sheria kwa sababu hakuwa akiripoti katika mamlaka ya magereza kama ilivyotakiwa, wakati alipokuwa Ujerumani kwa matibabu baada ya kupewa sumu. Tangu mwaka 2014, Navalny amekuwa akikabiliwa na kesi ya madai ya udanganyifu iliyokuwa imesimamishwa kwa muda na ambayo amesema imechochewa kisiasa.

Soma zaidi:Maelfu ya wafuasi wa Navalny wakamatwa Urusi

Kulingana na mawakili wake, huenda Navalny akatumikia kifungo cha miaka miwili na miezi minane kwa vile alishawahi pia kutumikia kifungo cha nyumbani siku za nyuma. Olga Mikhailova, ni mmoja wa mawakili wake:

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo na mahakama, Navalny alijitetea kwamba asingeweza kuripoti katika mamlaka ya magereza kama alivyotakiwa kisheria kwani alipoteza fahamu wakati akipelekwa Ujerumani kwa matibabu.

"Nilikuwa nikipatiwa matibabu Ujerumani," amesema Navalny akiwa mahakamani.

Lakini Jaji alisistiza kwamba alilazimika kutimiza masharti hayo katika hali yoyote ile.

"Mahakama imeamua kuunga mkono hoja ya Mamlaka ya Wafungwa," alisema jaji Natalya Repnikova wakati alitangaza uamuzi wa mahakama.

Makabiliano kati ya polisi na waandamanaji mjini Moscow, UrusiPicha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Navalny arudia kwamba alipewa sumu kwa amri ya rais Putin

Na kwa mara nyingine mkosoaji huyo wa Rais Vladimir Putin amezishutumu mamlaka za Urusi kwa kujaribu kumuua kwa kumlisha sumu ya Novichok inayoathiri Neva.

Navalny alirudi Urusi kutoka Ujerumani mapema mwezi huu, licha ya kuonywa kwamba atakamatwa mara baada ya kuwasili nchini humo. Tangu alipokamatwa, Urusi imeshuhudia maandamano makubwa ya watu wengi katika wikiendi mbili tofauti pamoja na watu kadhaa kukamatwa na polisi.

Serikali ya Urusi sasa inataka kutuma wanajeshi kulinda mashule ili kuhakikisha wanafunzi hawashiriki katika maandamano hayo ya kumuunga mkono Navalny.

Soma zaidi:Navalny akamatwa baada ya kutua Moscow

Mamalaka za Urusi zimekuwa zikijaribu kuzima maandamano hayo kwa njia yoyote iwezekanayo.

Na ndiyo maana zimeamua kuzilenga shule kwa vile waandamanaji wengi ni vijana wadogo.

Kulingana na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, vijana wa chini ya miaka 18 wapatao 205 walikamatwa kote Urusi katika maandamano ya Jumapili iliyopita.

Na maandamano zaidi yanatarajiwa kufanywa kufuatia hukumu hiyo ya mahakama dhidi ya Navalny.

Vyanzo: dpa, afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW