1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawazi Sharif amteuwa mdogo wake kumrithi

29 Julai 2017

Waziri mkuu aliendolewa nchini Pakistan Nawaz Sharif amemtaja ndugu yake Shahbaz, waziri kiongozi wa jimbo la Punjab, kuwa mrithi wake, na kumteuwa waziri wa zamani wa mafuta Shahid Khan Abbas kuwa waziri mkuu wa muda.

Pakistan Shabaz Sharif
Shahbaz Sharif ndiye kiongozi mkuu mpya wa chama cha Pakistan Muslim League - Nawaz. Shahbaz ni mdogo wake waziri mkuu alieondolewa Nawaz Sharif.Picha: picture alliance/dpaEPA/PMLN

"Namuunga mkono Shahbaz Sharif kuchukuwa nafasi yangu lakini itachukuwa muda kuwania uchaguzi hivyo kwa wakati huu nameteuwa Shahid Khaqan Abbas," alisema Sharif katika hotuba kwa chama chake iliotangazwa kupitia televisheni.

Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya mahakama ya juu kabisaa ya Pakistan kumuondoa madarakani Sharif kufuatia uchuguzi wa madai ya rushwa dhidi yake na familia yake, na kuhitimisha muhula wake wa tatu wa kihistoria madarakani.

Sharif mdogo anashikilia kiti cha ubunge wa jimbo tu, hivyo lazima achaguliwe kuingia bunge la taifa kabla ya kuweza kuwa waziri mkuu mpya. Abbas anatarajiwa  kama mshikiliaji wa nafasi hiyo katika kura ya bungeni, ambako chama cha Sharif cha Pakistan Muslim League - Nawaz kina wingi mkubwa katika baraza lenye jumla ya viti 342.

Upinzani huenda pia ukasimamisha mgombea kwa nafasi ya waziri mkuu, ingawa mteule wao ana nafasi finyu ya kupata kura za kutosha. Abbasi mwenye umri wa miaka 58 anaonekana kama mfuasi mtiifu kwa Sharif, na alikuwa waziri wa mafuta katika baraza la mawaziri lililopita.

Waziri mkuu wa muda alieteuliwa na Sharif, Shahid Khaqan Abbas.Picha: picture-alliance/dpaT. Mughal

Alia kufanyiwa mchezo mchafu

Katika mkutano huo wa chama Sharif pia ameelezea kusikikitishwa kwake na uamuzi wa mahakama wa kumuondoa madarakani na kuzitaja sababu za kuondolewa kwake kuwa zisizokuwa na msingi. Alisema upinzani ulikuwa unapiga kampeni dhidi yake katika siku za karibuni, ukimtuhumu yeye na familia yakekwa kujihusisha na madai ya rushwa.

Alisema mikono yake ni safi na hakuna kati ya wanafamilia yake alietumia vibaya fedha za serikali. Sharif alisema alishinikizwa na upinzani kujiuzulu lakini alikataa kukubaliana na matakwa yao kwa sababu aliamini madai yaliotolewa dhidi yake hayakuwa na msingi.

Nawaz Sharif amekuwa waziri wa 15 katika historia ya Pakistan ya miaka 70 -- ambayo karibu nusu yake imekuwa chini ya utawala wa kijeshi -- kuondolewa madarakani kabla ya kumaliza muhula kamili. Uamuzi huo ulishangiliwa na upinzani ulioingia mitaani na kugawa pipi na kupiga ngoma kusherehekea.

Mgawanyiko miongoni mwa raia

Lakini Wapakistan waligawanyika juu ya iwapo uamuzi huo umerudisha nyuma mchakato wa demokrasia nchini humo, ambapo wafuasi, wachambuzi na baadhi katika duru za habari wakikosoa uamuzi huo kama mapinduzi ya kimahakama.

Mahakama ilisema katika hukumu yake kuwa ilimuengua Sharif kwa kushindwa kuelezea mshahara wake wa kila mwezi wa dola 2,700 kutoka kampuni inayomilikiwa na mtoto wake wa kiume katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Maryam Nawaz, binti yake Sharif alietajwa katika nyaraka za Panama.Picha: Reuters/F. Mahmood

Nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa Sharif hakuchukuwa mshahara huo benki, lakini jopo la majaji watano lilisema kushindwa kwake kuelezea uwepo wa mshahara huo kulimaanisha kuwa hakuwa mwaminifu --- ambalo ni sharti kwa wanasiasa wa Pakistan chini ya katiba ya nchi hiyo.

Kiongozi wa upinzani Imran Khan, ambaye amekuwa akiongoza harakati dhidi ya Sharif, alisifu uamuzi huo na kusema unafungua ukurasa mpya nchini Pakistan. Lakini waangalizi waliikosoa na kuitaja kuwa ya kisiasa, ambapo mtetezi wa haki za binaadamu Asma Jahangir aliiambia televisheni binafsi ya Geo siku ya Ijumaa, kwamba jeshi lenye nguvu lilikuwa linazitumia mahakama kuvuruga demokrasia.

Mzozo kati yake na jeshi

Jeshi lilikuwa na uhusiano tata na Sharif, ambaye alichukuwa hatua kadhaa kurekebisha uhusiano na hasimu mkuu wa Pakistan anaemiliki silaha za nyuklia - India. Uhusiano wa Sharif na kampuni ya Umoja wa Falme za Kiarabu ulioneshwa kama sehemu ya uchunguzi katika madai ya rushwa dhidi ya familia yake yalioibuka kutokana na ufichuzi wa kile kilichojulikana kama nyaraza za Panama mwaka uliopita.

Sharif wakati akitoka kuhojiwa na kamati ya uchunguzi.Picha: Reuters/F. Mahmood

Uchapishaji wa nyaraka za siri zipatazo milioni 11.5 kutoka kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca zilionyesha biashara za nje za matajiri na wanasiasa wakubwa wa dunia uliwanasa watatu kati ya watoto wanne wa Sharif -- binti yake Maryam na vijana Hasan na Hussein.

Madai ya maisha ya anasa na majumba ya kifahari ya ukoo wa Sharif mjini London vilitawala kwa muda katika vyombo vya habari nchini humo. Hongo na aina nyingine za rushwa ni matatizo sugu nchini Pakistan. Chama cha PML-N kimekuwa kikikanusha mara kwa mara madai hayo, kikisisitiza kuwa utajiri wa ukoo huo ulipatikana kupitia biashara za familia ya Sharif nchini Pakistan na katika kanda ya Ghuba.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape,afpe

Mhariri: Lilian Mtono

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW