1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi 17 zinazochangia kutolipa kodi zaorodheshwa

6 Desemba 2017

Katika harakati za kukabiliana na ukwepaji kulipa kodi duniani, Umoja wa Ulaya umeziorodhesha nchi 17 zilizo nje ya Umoja huo na kuzitaja kama nchi zinazotoa nafasi ya uhalifu huo kufanyika.

Valdis Dombrovskis PK EU Kommission Brüssel
Picha: Reuters/Francois Lenoir

Lakini juhudi za Umoja huo kukabiliana na suala hilo zimeshutumiwa kutokana na kuwa hakuna hata nchi moja mwanachama wa Umoja huo iliyotajwa katika orodha hiyo iliyotolewa.

Mawaziri wa fedha wa Ulaya walitoa orodha hiyo Jumanne kufuatia miezi kadhaa ya malumbano na maombi ya dakika za mwisho ya baadhi ya mataifa kutaka yasitajwe. American Samoa, Bahrain, Barbados, Grenada, Guam, Korea Kusini, Macau, Visiwa vya Marshall, Mongolia, Namibia, Palau, Panama, Saint Lucia, Trinidad na Tobago, Tunisia na Milki za Kiarabu zote zilipatikana kutowiana na Umoja wa Ulaya katika masuala ya kodi.

Waliotajwa wamekataa kutoa ushirikiano

Makamu wa Rais wa Umoja wa Ulaya, Valdis Dombrovskis, alisema mbali na hizo nchi 17, zaidi ya nchi zengine 40 zinatazamwa kwa karibu hadi pale zitakadhamiria kufanya mabadiliko katika mifumo yake. Valdis alisema watazidisha shinikizo ili kulitokomeza suala hilo.

Valdis Dombrovskis (katikati) akizungumza na mawaziri wa fedha wa EUPicha: Reuters/F. Lenoir

Umoja wa Ulaya umesema wale waliotajwa wamekataa kutoa ushirikiano na kubadilisha mienendo yao baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mashauriano.

"Kuhusiana na hiyo orodha, ni nchi wanachama zinazostahili kutoa kauli kuhusiana na yatakayojiri, ila kama nilivyosema kuna orodha mbili, kuna orodha ya nchi 17 ambazo kwa sasa zimesemekana kuwa zisizotoa ushirikiano," alisema Valdis. "Lakini pia kuna orodha ya zaidi ya nchi 40 ambazo zimejitolea kufanya mamboa kadhaa kuhakikisha hazijumuishwi katika hiyo orodha ya awali," aliongeza Valdis.

Rais wa Panama Juan Carlos Varela amepinga kuwekwa kwa nchi yake katika orodha hiyo akisema inapiga hatua katika katika suala la kukwepa kulipa kodi. Umoja wa Ulaya lakini haujaamua ni adhabu gani zitakazotolewa kwa nchi zilizowekwa katika orodha hiyo.

Oxfam inasema hakuna nchi za EU zilizotajwa

Valdis amesema wale waliowekwa katika hiyo orodha ya pili yenye zaidi ya nchi 40, wamepewa muda ambao wanastahili kuhakikisha wanayatimiza masharti hayo.

Rais wa Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya Mario Daghi(kushoto) akiwa na ValdisPicha: Reuters/F. Lenoir

"Kwa nchi zilizostawi kiuchumi, zinatakiwa kutimiza masharti haya ndani ya mwaka mmoja na zile zinazostawi kiuchumi, zina miaka miwili kutimiza hilo,"alisema Valdis.

Lakini Shirika la kutoa misaada la Oxfam limeushutumu Umoja wa Ulaya kwa kutojumuisha nchi wanachama wake katika orodha hiyo. Katika ripoti iliyochapishwa na Shirika hilo kabla kutolewa kwa hiyo orodha, Oxfam ilitaja nchi nne za Umoja wa Ulaya inazoamini zingekuwa katika orodha hiyo iwapo zingekaguliwa kutumia vigezo vya Umoja huo.

Ilisema inaamini kwamba Luxembourg, Malta, Uholanzi na Ireland ni nchi ambazo hazingestahili kuachwa nje. Mshauri wa sera za Umoja wa Ulaya katika shirika hilo la Oxfam Aurore Chardonnet ameiambia DW, "ni vigumu sana kuziambia nchi zilizo nje ya Umoja wa Ulaya kujirekebisha wakati wewe mwenyewe hauezi kuipanga vyema nyumba yako."

Mwandishi: Jacob Safari/APE/DW

Mhariri: Mohammed Khelef