1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi kadhaa zasifu hatua ya Iran na Saudia kufufua uhusiano

Sylvia Mwehozi
11 Machi 2023

Nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Ufaransa zimekaribisha hatua ya Iran na Saudi Arabia kutangaza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia katika juhudi zilizosimamiwa na China.

China Treffen von Wang Yi, Ali Shamkhani und Musaad bin Mohammed Al Aiban
Picha: CHINA DAILY via REUTERS

Katika taarifa ya pande tatu iliyotolewa siku ya Ijumaa, Iran yenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Kishia na Saudi Arabia yenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisunni, zilitangaza kuwa zitafungua tena balozi ndani ya miezi miwili na kutekeleza mikataba ya usalama na ushirikiano wa kiuchumi iliyotiwa saini zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Ikulu ya Marekani White House imekaribisha makubaliano hayo, na kuongeza kuwa inasubiri kuona iwapo Wairani "watatimiza wajibu wao". Ufaransa pia imepongeza hatua hiyo, ikisema inaunga mkono mazungumzo, lakini imeitaka Iran "kuachana na vitendo vyake vya kuvuruga utulivu". Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha tangazo hilo na kusema bado yuko tayari "kutumia ofisi yake kuendeleza mazungumzo ya kikanda."

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: ATHIT PERAWONGMETHA/AFP/Getty Images

Mwanadiplomasia mkuu wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud alisema makubaliano hayo yanatokana na dhamira ya serikali ya Kifalme ya "suluhu za kisiasa na mazungumzo", mbinu ambayo inngependa kuwa ya kawaida katika eneo hilo.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesifu hatua hiyo akisema Tehran "itatayarisha kikamilifu mipango mingine ya kikanda. Kurejea kwa uhusiano wa kawaida kati ya Tehran na Riyadh kunatoa fursa kubwa kwa nchi hizo mbili, kanda na ulimwengu wa Kiislamu," alisema mwanadiploamsia huyo kupitia Twitter.

Soma pia: 

Iran yatumai kurejesha mahusiano na Saudi Arabia

Riyadh ilikata uhusiano na Tehran baada ya waandamanaji wa Iran kushambulia ofisi za kidiplomasia za Saudia mwaka 2016 kufuatia mauaji ya mhubiri wa Kishia mwenye ushawishi Nimr al-Nimr. Iran na Saudi Arabia zinaunga mkono pande tofauti zinazohasimiana katika maeneo kadhaa ya migogoro ikiwemo Yemen. Tehran inawaunga mkono waasi wa Kihuthi huku Riyadh inaongoza muungano wa kijeshi unaounga mkono serikali. Pande hizo mbili pia zinawania ushawishi nchini Syria, Lebanon na Iraq.

Zaidi ya waasi 150 wa Yemen wauawa katika mashambulizi Yemen

Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Tangazo la Ijumaa, linafuatia siku tano za mazungumzo ambayo hayakutangazwa hapo awali huko Beijing na duru kadhaa za mazungumzo nchini Iraq na Oman na linahitimisha juhudi za kupunguza hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Mshikamano kati ya Saudi Arabia, msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani, na Iran ambayo inavutana na nchi za Magharibi kuhusu mpango wake wa nyuklia, unaweza kurekebisha uhusiano katika kanda ya Mashariki ya Kati ambayo inakabiliwa na misukosuko kwa miongo kadhaa.

Iran yakaribisha mazungumzo na Saudi Arabia

Hatua ya Iran na Saudia kutangaza kurejesha uhusiano inakuja takribani miaka miwili na nusu baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo iko kati ya Saudi Arabia na Iran, kutia saini mkataba wa kurejesha uhusiano na Israel hatua ambayo haikutarajiwa.

Pia inafuata juhudi pana za usuluhishi wa mizozo ya kikanda, ikiwa ni pamoja na mvutano wa nchi za Ghuba na Qatar ambao ulianza Juni 2017 na kudumu hadi Januari 2021.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW