1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi karibu 200 zinashiriki mkutano wa mazingira Madrid

2 Desemba 2019

Wajumbe kutoka nchi takriban 200 wanakutana katika mkutano unaojadili mabadiliko ya tabia nchini mjini Madrid nchini Uhispania.

Logo COP 25 in Chile

Tarehe 3 Desemba unafanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira na mkutano huo hapana shaka unajikuta katikati ya maandamano ya ulimwengu mzima yanayofanywa na vuguvugu la maandamano la vijana, wanaodai kulindwa kwa mazingira.

Greta Thunberg mwanaharakati wa mazingira kijana kutokea Sweden alianza kwenda Chile ambako mwanzoni ndiko kulikopangwa kufanyika mkutano huo wa mazingira wa COP. Lakini sasa yuko njiani kurudi barani Ulaya akitumia mashua maalum isiyoharibu mazingira na hakutaka kusafiri kwa ndege kutoka Chile.

Mkutano huo ulishindwa kufanyika Chile kutokana na vurugu zilizozuka nchini humo na hivyo ukalazimika kuhamishiwa mjini Madrid na kwa maana hivyo Greta anasema anataka  akifika Ureno atumie njia ya barabara kuingia Uhispania.

Lakini ameandika kwenye ukurasa wa Twita kwamba safari yake inaelekea kuwa ya taratibu kuliko alivyofikiria. Licha ya mwendo huo wa kinyonga anatarajia mwanaharakati huyo kwamba hatua itapigwa katika mkutano huo wa mazingira.

Kauli za kutetea Juhudi za kulinda mazingira bado zinasikika barani Ulaya 

Waziri wa mazingira wa Ujerumani Svenja Schulze Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Kauli za kutetea juhudi zinazofanyika kulinda mazingira zimesikika tayari kutoka nchi kama Ujerumani ambako waziri wake wa mazingira Svenja Schulze anasema watu wanapaswa kwanza kushusha pumzi kwamba licha ya Chile kushindwa kuandaa mkutano huo, umepatikana mji wa kuandaa mkutano huo.

''Kwanza ninaishukuru sana Uhipania katika kipindi cha muda mfupi  inaweza kuandaa mkutano wa COP. Hiyo ni ishara kubwa muhimu inayoonesha mshikamano kwamba watu 20,000 mpaka 25,000 wanaweza kupokelewa Uhispania, hiyo ni ishara muhimu sana. Mkutano wa COP kwa hivyo unafanikiwa na tukiweza tutaendelea kuimarisha malengo yetu. Nchi zinapaswa kufanya zaidi kama zilivyoahidi,'' alisema Svenja Schulze.

Wakati nchi kiasi 190 ziliposaini mkataba wa mazingira wa Paris mwaka 2015 zote zililazimika kuridhia kupunguza gesi ya viwandani  ili kuzuia  kupindukia viwango vya nyuzi joto 2. Kila nchi ilitakiwa alau kuhakikisha zinapunguza ujoto kwa alau nyuzi joto 1.5 na kwa maana hiyo nchi zote hivi sasa  zinatakiwa ziwe tayari zimeimarisha mipango yao ya mazingira.

Wanasayansi wanaonya daima kwamba hatua hizo zinabidi zifanyika haraka na hasa kutoka na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameanza kushuhudiwa. Lakini ikiwa kuna malengo zaidi yanayoweza kufikiwa mjini Madrid bado hilo ni suala linalotiliwa mashaka.

Kufikia sasa ni nchi chache tu na hasa za Afrika na Asia ambazo zimeahidi kuchukua hatua zaidi kulinda mazingira. Mwanzoni mwa mwezi wa Novemba  rais wa Donald Trump ambaye  haamini juu ya  mabadiliko ya tabia nchi  hatimae alianzisha mchakato rasmi wa kuupiga kikumbo mkataba wa mazingira wa Paris.

Chanzo DW