1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi maskini zimeanza kulalamika Copenhagen

9 Desemba 2009

Pendekezo la Denmark kuhusu makubaliano ya Copenhagen limefichuka,Nchi za G77 zasema zinaonewa

Mkutano wa Copenhagen umeanza kuzusha hisia kali kutoka nchi maskiniPicha: AP

Mkutano wa Kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unaendelea katika mji mkuu wa Denmark Copehagen. Hata hivyo tayari kumezuka malalamiko katika mkutano huo kutoka upande wa nchi zinazoendelea baada ya pendekezo la Denmark kufichuka kabla ya wakati . Nchi zinazoendelea zimelishutumu pendekezo hilo na kulalamika kwamba linalenga kuzitia nchi hizo katika umaskini wa kudumu.Muswaada huo umefichuka kabla ya wakati wake na kusambazwa kwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huo. Hatua hiyo imeonekana kama suala ambalo linaweza kuyaweka pabaya mazungumzo ya Copenhagen.Nchi zinazoinukia kiuchumi za kundi la G77 zimeukosoa muswaada huo wa Denmark zikisema kwamba unazipendelea zaidi nchi tajiri katika masuala nyeti yanayohusu upunguzaji wa utoaji kiwango cha gesi zinazoharibu mazingira pamoja na ufadhili wa shughuli za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.Mjumbe kutoka Sudan Lumumba Stanislas Dia Pin ambaye anaongoza kundi hilo la G77 linalozijumuisha pia nchi mbili zinazochafua kwa kiasi kikubwa mazingira China na India,anasema mpango huo unakwenda kinyume kabisa na matakwa ya walio wengi na unatishia hatua ya kufikiwa makubaliano katika mkutano huo.Hata hivyo amesema kwamba nchi hizo hazitajiondoa kwenye mazungumzo katika wakati huu kwa sababu hawezi kukubali kushindwa,lakini kitakachofanyika ni kwamba hawatosaini makubaliano hayo.Na sababu ni moja anasema mjumbe huyo kwamba haiwezekani nchi maskini kusaini mpango ambao unaikandamiza asilimia 80 ya idadi jumla ya ulimwngu na kuitumbukiza katika mateso na kuinyima haki.Hata hivyo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akizungumzia kuhusu suala hilo la mabadiliko ya hali ya hewa amesema kwa upande wake anamatumaini makubwa kwamba mwafaka utafikiwa,zaidi ya hayo Ban Ki Moon amesema kwamba-

Suala la kupunguza viwango vya utoaji gesi inayoharibu mazingira kutoka viwandani linazusha mvutanoPicha: AP

''Kile kilichojitokeza hadharani kimezusha shakashaka kuhusu ujumbe mahsusi wa kisayansi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na ujumbe huo ni wazi kabisa kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanatokeo na kwa kasi zaidi kuliko tulivyotarajia na sisi binadamu ndio chanzo kikubwa.''

Matarajio ya kufikiwa makubaliano katika mkutano huo yalipata nguvu hapo jana wakati Marekani ilipotangaza kwamba itaanza kupunguza utoaji wa gesi ya Carbon Dioxide ambayo ni sumu kwa mazingira.Tangazo hilo lilitolewa na mjumbe wa Marekani katika kikao hicho Lisa Jackson.Rais Barack Obama anatazamiwa kuhudhuria mkutano huo katika kipindi cha mwisho.Juu ya yote lakini nchi zinazoendelea ambazo nyingi ndizo zinazochafua mazingira kwa kiasi kikubwa zinakataa kukubaliana na nchi tajiri kuhusu suala la upunguzaji kiwango cha utoaji wa gesi chafu kwa alau asilimia 40 kufikia mwaka 2020.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW