1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi wanachama wa UM walaani mashambulio ya Aleppo

16 Novemba 2016

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimelaani mashambulio yanayowalenga raia katika mji wa Aleppo, zimetaka hatua za haraka za kusitisha mapigano zichukuliwe ili kupisha mpango wa amani nchini Syria.

USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien
Picha: picture-alliance/dpa/M. Rajmil

Milio ya mabomu ilianza saa chache baada ya mazungumzo kwa njia ya simu baina ya rais Vladmir Putin wa Urusi na rais mteule wa Marekani Donald Trump. Katika mazungumzo yao viongozi hao walikubaliana juu ya kuendeleza kwa pamoja mapambano dhidi ya adui namba moja kama anavyoitwa na serikali ya Kremlin nchini Urusi wakimaanisha Ugaidi wa kimataifa na misimamo mikali.

Mashambulio hayo mapya ni ishara ya wazi kwa utawala wa rais  Barack Obama dhidi ya sera ya serikali yake kuhusu Syria. Mazungumzo ya muda mrefu baina Washington na Moscow yameshindwa kupata muafaka wa kumaliza mapigano nchini Syria. Urusi imesema kwamba kwa mara ya kwanza imetumia makombora yake ya masafa marefu kulenga mkoa wa Kaskazini wa Idlib na maeneo ya mkoa wa kati wa Homs lakini taarifa hiyo haikutaja mkoa wa Mashariki wa Aleppo.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: picture-alliance/dpa/R. Sitdikov

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema kwamba operesheni hiyo kubwa imehusisha mapambano yaliyolenga maeneo yanayoshikiliwa na waasi wa makundi ya Dola linalojiita la Kiislamu IS na kundi linalofungamana na Al Qaeda katika mikoa ya Idlib na Homs.

Kura iliyofanyika katika Umoja wa mataifa ilifwatia azimio lililopendekezwa na Saudi Arabia nchi ambayo inawaunga mkono waasi nchini Syria. Nchi 116 zilipiga kura kuunga mkono azimio linalotaka njia za haraka zipatikane ili kusitisha mapigano yanayolenga hasa maeneo ya wapinzani nchini Syria, nchi 15 zilipinga hoja hiyo na nchi 49 hazikushiriki kabisa katika zoezi hilo. Wajumbe wa Urusi na Iran ambao wanawakilisha nchi ambazo ni washirika wakuu wa rais Bashar al Assad walikuwa miongoni mwa nchi 15 ambazo zilipinga azimio hilo.

Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa Abdallah Al Mouallimi aliziomba nchi nyingi ziunge mkono azimio alilopendekeza huku akitumia shairi katika hotuba yake lililokumbushia mtoto wa Kisyria Aylan Kurdi ambae picha zake zilitanda kwenye vyombo vya habari pale mwili wa mtoto huyo ulipoonyeshwa ukiwa katika fukwe ya bahari huko nchini Uturuki.  Kwa upande wake balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jaafari alimwambia mwenziwe huyo kuwa serikali ya Saudi Arabia ndio ingekuwa ya mwisho kuzungumzia kuhusu haki za binadamu huku akiitetea serikali yake ya Syria kuwa inapambana na Ugaidi.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE 

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW