1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za GCC zaipuuza Marekani na kujisogeza zaidi kwa China

9 Desemba 2022

Rais wa China akaa chini na viongozi wa Ghuba katika mkutano wa kilele wenye lengo la kuimarisha zaidi mahusiano ya kiuchumi baina ya pande hizo mbili

Saudi-Arabien Riad | Kronprinz Mohammed Bin Salman empfängt Xi Jinping
Picha: Bandar Algaloud/Saudi Royal Court/REUTERS

China na Saudi Arabia kwa mara nyingine zimethibitisha umuhimu wa kuweko uthabiti katika masoko ya mafuta duniani pamoja na dhima ya Saudi Arabia katika suala hilo. Hilo ni tamko la pamoja lililotolewa leo Ijumaa kufuatia ziara ya rais wa Chin Xi Jinping nchini Saudi Arabia.

Rais wa China Xi Jinping ambaye aliwasili toka Jumatano nchini Saudi Arabia  Alhamisi alikutana na mwenyeji wake mfalme Salman na mwanawe mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Mohammed Bin Salman na pia viongozi wengine kadhaa kutoka ulimwengu wa Kiislamu, kuanzia Misri, Palestina, Sudan mpaka Kuwait.

Ijumaa imetolewa taarifa ya pamoja baada ya rais huyo wa China kukutana na viongozi wa Riyadh ambapo, miongoni mwa mwengine, taarifa hiyo imesema Jamhuri ya watu wa China inaikaribisha dhima ya Saudi Arabia kama muungaji mkono wa urari na uthabiti wa soko la mafuta duniani na vile vile kama msafirishaji mkubwa wa kutegemewa kwa China.

Picha: Bandar Algaloud/Saudi Royal Court/REUTERS

Nchi za Kiarabu za Ghuba ambazo ni washirika wa kimkakati wa Marekani sasa zinaimarisha mahusiano na China ikiwa ni sehemu ya kuigeukia zaidi mashariki katika kuimarisha uchumi wa mataifa yao unaotegemea nishati. 

Mikataba 46 na maelewano kadhaa yamefikiwa katika masuala mbali mbali kuanzia masuala ya ujenzi wa makaazi mpaka mafunzo ya lugha ya kichina. Hata hiyvo, kuna machache sana yaliyowekwa wazi juu ya mikataba hiyo licha ya vyombo vya habari vya Saudia kusema inagharibu zaidi ya dola bilioni 30.

Picha: Bandar Al-Jaloud/AFP

Wakati unafanyika mkutano wa kilele kati ya nchi hizo za Ghuba na China hii leo huko Riyadh kuna maeneo kadhaa muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi sita wanachama wa baraza la ushirikiano la Ghuba pamoja na China,nchi ambayo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.

Itakumbukwa kwamba kufikia mwaka 2020 China iligeuka kuwa mshirika mkubwa kabisa wa kibiashara na nchi hizo za GCC na hasa katika nyanja ya nishati,ikiagiza petroli na gesi kutoka Oman,Umoja wa Falme za kiarabu,kuwait na Saudi Arabia ambako asilimia 17 ya nishati ya mafuta ya China iliagizwa kutoka huko katika mwaka 2021.

Qatar inaiuzia China gesi asilia ya kimiminika, biashara ambayo imeongezeka zaidi kufuatia mgogoro wa nishati unaoikabili dunia kufuatia vita nchini Ukraine.

Picha: Saudi Press Agency/AP/picture alliance

Na zaidi ya hilo ikumbukwe Julai mwaka 2004 China na nchi za GCC ziliwahi kutangaza kuanzisha majadiliano ya kutafuta makubaliano ya biashara huria lakini kiasi miongo miwili baadae na baada ya kufanyika duru tisa za mazungumzo  pande hizo mbili bado hazijafikia makubaliano ya mwisho licha ya kutolewa ahadi mwezi Januati ya mchakato huo kuongezwa kasi.

Kwahivyo mkutano wa leo kati ya nchi hizo za Ghuba na China kwa kiasi kikubwa unaonekana kama ni fursa ya kuyafufua tena mazungumzo hayo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW