1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Ghuba zapinga Golan kutambuliwa kuwa chini ya Israel

Angela Mdungu
26 Machi 2019

Saudi Arabia, Kuwait na Bahrain zimeungana na nchi nyingine, kulaani hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kuitambua Milima ya Golan kama sehemu ya Israel

Israel - Syrien Golan-Höhen
Picha: Getty Images/AFP/J. Eid

 Kauli za nchi hizo kupitia vyombo vya habari zimetolewa siku chache baada ya nchi za Iran na Uturuki kulaani pia ahadi ya Trump.

Saudi Arabia imesema, jaribio la kutaka kulihalalisha eneo la Golan kama sehemu ya Israel halibadili ukweli na kwamba milima inatambuliwa na azimio la umoja wa Mataifa kuwa ni ardhi halali ya nchi ya kiarabu ya Syria.Ripoti hiyo imeongeza kuwa hatua ya Rais Trump itakuwa na madhara makubwa katika mchakato wa kuleta amani Mashariki ya kati na kwa ulinzi na utulivu wa eneo hilo.

Nayo Kuwait kupitia shirika lake la habari imeonesha kuchukizwa kwake na hatua ya Rais wa Marekani na kusema imevunjwa moyo na kukatishwa tamaa kwa uamuzi huo. Kwa upande wake Bahrain imesema inalitambua eneo la Golan kama eneo la Syria na si vinginevyo.

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/L. Mills

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akiipa shinikizo Marekani kutambua  milima ya Golan kama eneo la Israel kwa madai kwamba mahali ilipo milima hiyo ni  muhimu kwa mikakati na Usalama wa Israel na uthabiti wa Kanda nzima. Akionesha furaha yake baada ya hatua ya Trump Netanyahu amesema, "Ninarejea sasa kutoka kwenye ziara ya kihistoria mjini Wshington. Kukubali kwa Rais Trump kutambua uhuru wetu juu ya milima ya Golan kutakumbukwa na vizazi vijavyo. Kuna kanuni moja muhimu katika maisha ya kimataifa-unapoanzisha vita vya uchokozi unapoteza miliki yako, usirudi na kuitaka tena baadaye.Ni mali yetu. Tuna misingi ya kihistoria kwenye milima ya Golan. Ukichimba pale utaona masinagogi ya kushangaza ambayo sasa tunayaboresha.''

Mashambulizi yaendelea ukanda wa Gaza

Wakati huohuo vikosi vya Israel vimeendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza zikiwemo ofisi za kiongozi mkuu wa kundi la Hamas. Mashambulizi hayo yamefanywa baada ya shambulizi la roketi linalodaiwa kutoka upande wa Palestina kupiga upande wa Israel. Akizungumzia mashambulizi hao wakati akiwa kwenye mkutano katika ikulu ya White house nchini Marekani waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake haiwezi kuvumilia mashambulizi hayo huku taarifa ya jeshi la nchi hiyo likidai kwamba takribani mashambulizi 30 ya roketi yalielekezwa upande wa Israel.

Mashambulizi kadhaa ya anga katika ukanda wa Gaza yaliibuka siku ya jumatatu na taarifa za awali hazijaonesha kuwepo kwa majeruhi.

Mwandishi: Angela Mdungu/DPAE/RTRE

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW