1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kigeni zapeleka misaada Somalia baada ya shambulizi

Caro Robi
17 Oktoba 2017

Somalia inahitaji kwa dharura damu kuwatibu waathiriwa wa shambulizi la mabomu yaliyofanyika Mogadishu ambapo watu zaidi ya 300 waliuawa na wengine takriban 400 walijeruhiwa.

Somalia Mehr als 260 Tote nach Doppel-Anschlag in Mogadischu
Picha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Waziri wa habari wa Somalia Abdirahman Omar Osman amesema nchi yake haina akiba ya damu hospitalini na mfumo duni wa huduma za afya unatatiza utaoji wa matibabu na kuongeza mbali na kuomba msaada wa damu pia wanahitaji msaada katika kuzitambua maiti.

Somalia yahitaji misaada

Osman amesema zaidi ya miili 100 iliyozikwa jana ilikuwa imeungua kiasi cha kutotambulika na anatumai miili mingine itaweza kutambuliwa. Madaktari wa Uturuki wengi wao wataalamu wa upasuaji na wataalamu wa majeraha ya uti wa mgongo waliwasili jana pamoja na waziri wa afya wa Uturuki.

Raia wakikimbia kutoka eneo la mkasa mjini MogadishuPicha: Reuters/F. Omar

Naibu wa waziri mkuu wa Uturuki Recep Akdag amewaambia wanahabari baada ya kurejea kutoka Somalia kuwa wamewasafirisha waathiriwa 35 walio katika hali mahututi hadi Ankara kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

Qatar nayo imewasafirisha kwa ndege waathiriwa wengine 25 na kuwapeleka katika hospitali za Sudan. Nchi jirani za Djibouti na Kenya pia zimewasilisha misaada ya kutoa matibabu. Kundi la madakatari kutoka Djibouti liko Mogadishu kuwatibu majeruhi na kusaidia katika kuwasafirisha kuelekea Djibouti.

Kenya pia itawasafirisha majeruhi 31 hadi Nairobi kwa matibabu maalum na imewasilisha tani 11 za dawa na vifaa vya matibabu kwa Somalia. Ndege ya kijeshi ya Marekani imetua mjini Mogadishu leo ikiwa imebeba vifaa vya matibabu na misaada ya kiutu.

Maafisa wa Somalia wamesema watu kadhaa bado hawajulikani waliko na idadi ya waathiriwa inatarajiwa kuongezeka kufuatia shambulizi hilo baya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi kirefu.

Al Shabab yashukiwa kuhusika

Nchi mbali mbali duniani zikiwemo Marekani, Ujerumani, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimelaani shambulizi hilo zikilitaja la kinyama na lililofanywa na waoga.

Raia wa Somalia wakiandamana kulaani mashambuliziPicha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Serikali ya Somalia inalishutumu kundi la Al Shabab, kundi la waasi wenye mafungamano na wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la Kiislamu IS na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda kwa shambulizi hilo. Hata hivyo kundi hilo mpaka sasa halijadai kuhusika na shambuli hilo.

Wachambuzi wanasema hakuna shaka kuwa Al Shabab ndilo lililohusika kwani hakuna kundi jingine nchini Somalia lililo na uwezo wa kufanya shambulizi kubwa la namna hiyo. Al Shabab imefanya uasi nchini humo kwa zaidi ya muongo mmoja mara nyingi ikiyalenga maeneo muhimu mjini Mogadishu.

Shambulizi hilo la Jumamosi limedidimiza matumaini ya taifa hilo kujikwamua kutoka mashambulizi ya mara kwa mara, na imeibua maswali kuhusu uwezo wa serikali ya Somalia inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kutoa usalama kwa raia wake.

Nchi hiyo inayoorodheshwa miongoni mwa masikini barani Afrika, inakumbwa pia na uhaba wa chakula na inategemea pakubwa misaada ya kigeni katika karibu kila nyanja.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri:Gakuba, Daniel