1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Nchi za kigeni ziko mbioni kuwaondoa raia wao Sudan

24 Aprili 2023

Serikali za nchi za kigeni zinaendelea kuondowa raia wao Sudan huku maelfu ya Wasudan wenyewe wakihatarisha maisha yao kukimbilia katika nchi jirani.

Sudan | Proteste in gegen die Militärherrschaft Khartoum
Raia wa Sudan wakiandamana kupinga utawala wa kijeshiPicha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Nchi za ulimwengu tangu zile za barani Ulaya, Marekani, Asia, Mashariki ya Kati hadi Afrika zikichukua juhudi za kuondowa raia wao, Wasudan wenyewe pia wanapambana kuikimbia nchi yao kutafuta usalama kwa majirani.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya shughuli za kuratibu misaada ya kiutu, OCHA imesema raia wa Sudan wanayakimbia maeneo yaliyoathirika kwa vita wakielekea katika nchi kadhaa  Jirani ikiwemo Chad, Misri na Sudan Kusini,lakini pia maelfu ya wakimbizi wamekusanyika pia kwenye mpaka na Ethiopia.

Soma zaidi:Nchi za Kigeni zaondosha raia wake Sudan 

Makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa na makundi yaliyoko vitani kupitisha sikukuu ya Eid al Fitri ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambayo yamekuwa yakitekelezwa kwa muda tangu siku ya Ijumaa yanatarajiwa kumalizika jioni ya leo Jumatatu ambapo huenda vita vikaanza upya na mapigano kuchachamaa.

Sudan Kaskazini ambayo kwa miaka imekuwa ikiyumba kisiasa sasa inashuhudia majenerali wake wawili wenye nguvu kubwa pamoja na makundi yao ya kijeshi wameingia kwenye vita kubwa ya mapambano ya kuwania madaraka katika kipindi cha zaidi ya wiki sasa.

Rais Abdel Fatah al Burhani ambaye pia ni kamanda mkuu wa jeshi la Sudan akiwa pamoja na jeshi la taiafa anapambana dhidi ya makamu wake Mohammed Hamdan Daglo, kiongozi wa kundi kubwa lenye nguvu la wanamgambo linalofahamika kama Rapid Support Forces-RSF.

Wote wawili hao walikuwa wakishirikiana kuiongoza nchi hiyo yenye utajiri wa dhahabu na mafuta yenye wakaazi milioni 46 tangu mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021.

UN: Zaidi ya watu 400 wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa vita hivyo

Wanajeshi wa kikosi cha msaada wa dharura RSF wakishika doria katika wilaya ya Nile Mashariki, Sudan.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa unasema kiasi watu 427 wameuwawa japo idadi inawezekana ikawa ni kubwa kuliko iliyotajwa. Na kuna wengine 3,700 waliojeruhiwa tangu vilipozuka vita hivyo. Hali ya usambazaji mahitaji muhimu katika mji wa Khartoum imekuwa mbaya kwa kiasi kikubwa,wakaazi wakitajwa kuhangaika kutokana na ukosefu wa maji na chakula huku pia kukatika kwa umeme kukitatiza mawasiliano.

Uporaji unatajwa kuwa kitisho kikubwa. Wakati huohuo serikali nyingi za kigeni zinaendelea kuondowa raia wao.Nigeria inapanga kuanza operesheni ya kuondowa kiasi raia wake 3000 wengi wakiwa ni wanafunzi kupitia usafiri wa magari kuelekea Misri wiki hii.

Soma pia: Papa Francis ahimiza mazungumzo kumaliza mzozo wa Sudan

Mkurugenzi wa shirika linalosimamia masuala ya dharura Nigeria NEMA,Onimode Bandele amesema bado hakuna raia wa Nigeria aliyeondolewa lakini tayari upo mpango wa kutuma magari kuanza safari kesho kwa raia wake wakiwemo familia za wafanyakazi wake wa ubalozi. Afrika Kusini imesema hii leo kwamba imeshaanza kuwaondoa raia wake chungunzima wakiwemo wafanyakazi katika ubalozi wake, walionasa kwenye vita nchini Sudan.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini Clayson Monyela ameliambia shirika la habari la AFP kwamba raia wake wanapelekwa katika nchi jirani ingawa hakutaja nchi gani wala kusema lini wanatarajiwa kuwasili Afrika Kusini.

Awali Rais Cyril Ramaphosa aliwaambia waandishi habari mjini Johannesberg kwamba Waafrika Kusini wapatao 77 wamekwama Sudan lakini serikali yake imekubali pia kuwaondowa raia wa nchi nyingine waliokwama Sudan.

Afrika Kusini imejiunga na nchi nyingine nyigi za Ulimwengu zinazopambana kuharakisha operesheni ya kuondowa raia wao na kuwapeleka maeneo salama kufuatia vita nchini Sudan.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW