1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi zenye vikosi Afrika Magharibi na Kati

Josephat Charo
26 Septemba 2023

Ufaransa itawaondoa wanajeshi wake kutoka Niger kufikia mwisho wa 2023 kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai. Je ni nchi zipi za Magharibi zenye wanajeshi wake katika eneo la Afrika Magharibi na Afrika ya kati?

Niger Niamey | französische Luftwaffenbasis
Picha: ALAIN JOCARD/AFP/Getty Images

Niger, mshirika muhimu wa nchi za Magharibi katika mapambano dhidi ya uasi wa wanamgambo wa kiislamu katika eneo la Sahel, imewakaribisha wanajeshi wa nchi kadhaa za kigeni. Idadi ya nchi za kigeni zimeongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kufuatia mapinduzi katika nchi jirani za Mali na Burkina Faso, ambayo yamevuruga mahusiano kati ya nchi hizo na washirika wao wa Magharibi.

Ufaransa

Ufaransa ina vikosi 1,500 nchini Niger, vikisaidiwa na ndege zisizorushwa na rubani na ndege za kivita. Ilikuwa na vikosi vya kupambana an uasi Afrika Magharibi kwa muongo mmoja, lakini ikaigeukia Niger kuwaweka idadi kubwa ya wanajeshi wake kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi jirani za Mali na Burkina Faso mnamo 2021 na 2022 mtawalia.

Utawala wa kijeshi uliomuondoa madarakani rais wa Niger, Mohamed Bazoum, mnamo Julai 26 umefuta mkurururo wa mikataba ya kijeshi na Ufaransa.

Kabla mapinduzi hayo, Ufaransa ilipania kuepusha ukosoaji ambao ungejitokeza kuhusu jukumu lake katika eneo la Sahel na kupunguza kauli na fikra za kuipinga Ufaransa kwa kubadilisha muelekeo wake na kuvisaidia vikosi vya nchi za eneo hilo badala ya wanajeshi kutoka nchi za Magharibi kufanya kazi kubwa katika uwanja wa vita.

Ufaransa ingali ina kambi zake za kijeshi nchini Chad, ambako kuna vikosi 1,000, Ivory Coast vikosi 900, Senegal vikosi 350, na Gabon vikosi 400. Baadhi ya kambi hizi zinageuzwa kuwa operesheni za pamoja na majeshi ya mataifa hayo, kupunguza jukumu kubwa la Ufaransa.

Wanajeshi wa Burkina Fasio na Niger wakíhudhuria mafunzo ya kijeshi ya kila mwaka yaliyoongozwa na Marekani huko Jacqueville, Machi 14, 2023. Picha: Issouf Sanogo/AFP

Marekani

Marekani ina vikosi vyake takriban 1,100 nchini Niger ambako jeshi la Marekani linaendesha harakati zake katika kambi mbili. Mnamo 2017 serikali ya Niger iliridhia matumizi ya ndege zisizoendeshwa na rubani za Marekani kuwalenga na kuwashambulia wanamgambo. Haijabaikika wazi kiwango ambacho Marekani imetoa kama msaada wa usalama. Ubalozi wa Marekani mjini Niamey mwaka 2021 ulisema wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon na wizara ya mambo ya nje zilikuwa zimeipa Niger zaidi ya dola milioni 500 kwa ajili ya vifaa na mafunzo tangu mwaka 2012.

Soma pia: Ufaransa kuwaondoa wanajeshi wake Niger

Ujerumani

Kufikia Septemba 20, Ujerumani ambayo inawaondoa wanajeshi wake waliokuwa nchini Mali wakihudumu katika tume ya amani ya Umoja wa Mataifa, MUNISMA, ilisema vikosi 887 wangali bado wako Mali wakiwemo 755 katika mji wa kaskazini wa Gao, na wengine katika mji mkuu, Bamako. Kiasi vikosi 110 vya Ujerumani viko katika mji mkuu wa Niger, Niamey.

Italia

Italia ilikuwa na wanajeshi wapatao 300 nchini Niger kabla mapinduzi, kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo. Mnamo Agosti 6, wizara ya ulinzi ya Italia ilisema wanajeshi wake 65 walikuwa wameondoka Niger kutumia ndege ya kijeshi, wakati ilipotaka kutoa nafasi katika kambi yake ya kijeshi kwa raia ambao huenda wakahitaji msaada. Hii iliwaacha vikosi 250 wakiendelea kuhudumu katika operesheni ya kupambana na uasi na katika ujumbe wa kutoa mafunzo ya kijeshi Niger.

Umoja wa Ulaya

Umoja wa Ulaya una vikosi kati ya 50 na 100 wanaohudumu kwa miaka mitatu katika tume ya mafunzo ya kijeshi iliyoianzisha nchini Niger mnamo Desemba mwaka uliopita kuisaidia nchi hiyo kuboresha uratibu wake na miundombinu.

(reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW