1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za NATO zakubaliana kuondoka Afghanistan

15 Aprili 2021

Nchi za Muungano wa Kujihami wa NATO zinapanga kushirikiana katika kuondoa majeshi yake Afghanistan, baada ya Marekani kutangaza itafikisha mwisho, "vita virefu zaidi ilivyoshiriki Marekani" mnamo Septemba 11.

NATO-Abzug aus Afghanistan beginnt am 1. Mai
Picha: Johanna Geron/AFP/Getty Images

Muungano wa kujihami wa NATO tayari umeanza kufanya maandalizi ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Afghanistan. Mawaziri wa muungano huo wa kujihami wamejadili na kuafikiana kushirikiana katika kuwaondoa wanajeshi hao kuanzia Mei mosi na kumaliza shughuli hiyo miezi michache baadae.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema muungano huo utaendelea kusimama na Afghanistan na kwamba huu ni mwanzo mpya katika uhusiano wao.

Marekani imeshatimiza lengo lake Afghanistan

"Kuondoka kwetu Afghanistan kutakuwa kwa mpango, ushirikiano na hiari. Tunapanga kukamilisha kuwaondoa wanajeshi wetu wote katika kipindi cha miezi michache. Mashambulizi yoyote ya Taliban kwa vikosi vyetu yatajibiwa kwa nguvu zote," alisema Stoltenberg.

Majeshi ya Marekani AfghanistanPicha: Hoshang Hashimi/AP Photo/picture alliance

Usiku wa Jumatano Rais Joe Biden alitoa tamko rasmi mjini Washington kuhusiana na suala hilo akisema Marekani inafikisha mwisho "vita vyake vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi." Biden amesema kwamba Marekani imeshatimiza lengo lake Afghanistan.

"Kwa sasa mimi ni rais wa nne wa Marekani kusimamia uwepo wa majeshi ya Marekani Afghanistan, Warepublican wawili na Wademocrat wawili, sitopeana jukumu hili kwa rais wa tano wa Marekani. Baada ya kujadiliana kwa karibu na marafiki, washirika wetu, wakuu wetu wa jeshi, wakuu wa ujasusi, wanadiplomasia wetu, bunge la congress, makamu wa rais pamoja na Ashraf Ghani, nimeamua kwamba ni wakati wa majeshi ya Marekani kurudi nyumbani," alisema Biden.

Vikosi vya Afghanistan vina uwezo wa kuwalinda raia wake

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amezungumza na Rais Biden pia kuhusiana na hatua hiyo ya kuwaondoa wanajeshi hao. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffan Seibert, amesema viongozi hao wawili wamedhamiria kushirikiana kwa karibu katika masuala ya sera zao kuihusu Afghanistan.

Rais Ashraf Ghani wa AfghanistanPicha: Official Page for the President of The Islamic Republic of Afghanistan

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wa Twitter amesema baada ya kuzungumza na Rais Biden, Afghanistan inauheshimu uamuzi huo na kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vya Afghanistan vina uwezo kamili wa kuwalinda watu wake na nchi yao.

Kwa sasa kuna karibu wanajeshi 10,000 wa NATO na mataifa washirika nchini Afghanistan. Marekani iliivamia nchi hiyo mwaka 2001 baada ya mashambulizi ya Septemba 11 na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda. Nchi zengine za muungano wa NATO zilituma wanajeshi wake pia wakati huo katika nchi hiyo iliyo kusini mwa bara Asia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW