Nchi za NATO kuimarisha utengenezaji silaha Ukraine
26 Novemba 2024Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, alisema Ujerumani na nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO wanapanga kuimarisha utengenezaji wa silaha ndani ya Ukraine kujibu hatua za Urusi katika vita vinavyoendelea. Pistorius aidha amesema utengenezaji na manunuzi ya droni zinazoendeshwa kutumia akili mnemba ni jambo la kipaumbele, pamoja na ushirikiano mzuri zaidi kusaidia utengenezaji wa silaha.
Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani alisema Ukraine lazima iweze kuchukua hatua katika nafasi imara ya kuwa na nguvu, akisema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umechukua muelekeo wa kimataifa akirejelea wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 10,000 kutoka Korea Kaskazini ambao rais wa Urusi Vladimir Putin amewaleta nchini mwake kuwapa mafunzo ili wakapigane nchini Ukraine. Waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov ameunganishwa kwenye mkutano wa Berlin kwa muda wa nusu saa.
Waziri Pistorius alisema hatua ya Urusi kuishambulia Ukraine kutumia kombora jipya la masafa ya kati, ambalo lina athari za kiusalama kwa baraza zima la Ulaya, imekuwa na dhima muhimu wakati wa mazungumzo ya mjini Berlin.
Soma pia: Blinken akutana na mkuu wa jumuiya ya NATO
Pistorius pia alisema hatua za Urusi nchini Ukraine zinawaathiri watu nchini Ujerumani na nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya NATO na bila kujali ikiwa asilimia 2, 2.5 au 3 ya pato jumla la kitaifa litatumiwa kwa ajili ya ulinzi siku za mbele, lengo la nchi wanachama wa NATO ni kuziba mapengo ya mapungufu ya uwezo wa kiulinzi ili kuhakikisha uthabiti katika kuepusha mashambulizi.
Ufaransa kupeleka mfumo wa ulinzi wa ulinzi wa makombora Ukraine
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Sébastien Lecornu alisema Ufaransa itapeleka mfumo wa ulinzi wa anga wa Mistra dhidi ya makombora ya masafa mafupi nchini Ukraine katika wiki zijazo. Amesema wanahitaji kutafakari upya muelekeo kuhusu usalama na ulinzi katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 ijayo na kiwango cha matumizi ya asilimia mbili lazima kifikiwe, lakini pia ni muhimu kutumia fedha vizuri.
Waziri wa ulinzi wa Poland Wladyslaw Kosiniak-Kamysz kwa upande wake alisema nchi yake itatumia asilimia 4.2 ya pato jumla la kitaifa kwa ajili ya ulinzi mwaka huu na kwamba kiwango hiki kitaongezwa hadi asilimia 4.7 mwaka ujao. Waziri Wladyslaw pia amesema, "Leo tunakabiliwa na kitisho kikubwa kabisa tangu vita vikuu vya pili vya dunia. Leo tungali tuna muda. Hivi punde muda utatutupa mkono."
Mawaziri hao wa ulinzi pia walikutana chini ya kiwingu cha kurejea madarakani rais wa Marekani na mkosoaji mkubwa wa jumuiya ya NATO, Donald Trump. Trump ambaye anatarajiwa kuapishwa Januari 20 mwakani, ameitaka Ulaya iwekeze fedha zaidi katika usalama wake na anatarajiwa kupunguza msaada wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine.
Kufuatia ridhaa ya hivi karibuni ya Marekani na Uingereza, Ukraine imeanza kutumia makombora yaliyotengenezwa nchini Marekani chapa ATACMS na makombora ya Uingereza, Storm Shadow, kuyalenga maeneo ya kijeshi nchini Urusi.
Rais Putin alijibu kwa kuagiza shambulizi la kombora katika mji wa Ukraine wa Dnipro, ambao una idadi jumla ya wakazi zaidi ya milioni moja, kwa kutumia kombora jipya la masafa ya kati Alhamisi asubuhi wiki iliyopita. Alilipongeza jaribio la kombora hilo chapa Oreshnik na alisema litatengenezwa kwa wingi.
Urusi inasema kombora hilo linasafiri kwa kasi kubwa sana, kiasi cha kuifanya kuwa vigumu kwa mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora kulitungua. Wataalamu wanasema kombora hilo huenda kiufundi pia likawekewa kichwa cha nyuklia.
(dpa)