1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Ulaya kupunguza matumizi ya gesi ya Urusi

26 Julai 2022

Serikali za Umoja wa Ulaya zinakaribia kufikia makubaliano kuhusu mgawo wa gesi asilia katika msimu ujao wa baridi ili kujilinda dhidi ya hatua yoyote za kupunguzwa zaidi bidhaa hiyo na Urusi

Deutschland | Gas Pipeline Nord Stream 1
Picha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya wanajadiliana kuhusu rasimu ya sheria ya Ulaya ambayo itazihitaji nchi wanachama kupunguza mahitaji ya gesi asilia kwa asilimia 15 kutoka mwezi Agosti hadi Machi. Hii itahusu hatua za hiari za kupunguza matumizi ya gesi na, kama hilo halitaleta tija, basi kutawekwa hatua za lazima kote katika umoja huo wenye nchi 27 wanachama.

Soma pia: Urusi yaanza tena kusukuma gesi barani Ulaya

Hapo jana, kampuni kubwa ya nishati ya Urusi Gazprom ilisema itapunguza usambazaji gesi katika Umoja wa Ulaya kupitia bomba la Nord Stream 1 kwa hadi asilimia 20 ya uwezo wake, tangazo lililosababisha wasiwasi kuwa Rais wa Urusi Vladmir Putin atatumia biashara ya gezi katika kupinga upinzani wa Umoja wa Ulaya kwa vita nchini Ukraine.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amemshutumu rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kucheza mchezo wa kihuni na kujaribu kudhoofisha msaada mkubwa inaopatiwa Ukraine. Wiki iliyopita bomba la Nord Stream 1 lilifunguliwa tena baada ya kuwa limefungwa kwa siku 10 za ukarabati. Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya Nishati Kadri Simson amesema wanapaswa kuwa tayari kwa lolote.

Natarajia kamba mwisho wa siku tutakuwa na makubaliano ya kisiasa. Tunafahamu kuwa hakuna sababu ya kiufundi ya kufanya hivyo. Hii ni hatua iliyochochewa kisiasa na tunapaswa kuwa tayari kwa hilo.

Gesi asilia hutumika katika viwanda, kuzalisha umeme na kupasha joto majumbani wakati wa msimu wa baridi, na wasiwasi unaongezeka kuhusu uwezekano wa mdororo wa uchumi kama Ulaya haitahifadhi gesi ya kutosha na mgawo unahitajika ili kuimudu miezi ya baridi.

Kamishna wa Ulaya kuhusu masuala ya nishatiPicha: GEORG HOCHMUTH/APA/AFP/Getty Images

Halmashauri Kuu ya Ulaya inawashinikiza mawaziri wa nishati kufikia makubaliano ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya kuliharakisha pendekezo hilo la mgawo wa gesi.

Lakini Uhispania na Ureno zinasema zitapinga pendekezo la kupunguzwa kwa lazima, zikitaja usambazaji mdogo wa nishati katika maeneo mengine ya Ulaya na matumizi ya gesi ya Urusi ambayo yako chini mno ukilinganisha nan chi kama vile Ujerumani na Italia.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari na nchi za Magharibi zikajibu kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi, nchi 12 za Umoja wa Ulaya ama zimekatiwa au kupunguziwa gesi ya Urusi.

Ijapokuwa umeafikiana kupiga marufuku ya Mafuta na makaa ya mawe kutoka Urusi kuanzia baadae mwaka huu, Umoja wa Ulaya umejiepusha na kutangaza vikwazo dhidi ya gesi asilia ya Urusi kwa sababu Ujerumani, Italia na baadhi ya mataifa wanachama yanategemea pakubwa bidhaa hiyo.

AFP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW