1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zenye silaha za nyuklia zinazifanya za kisasa: SIPRI

Daniel Gakuba
17 Juni 2019

Nchi zenye silaha za nyuklia zinazidi kuzifanya za kisasa, licha ya kupungua kwa idadi ya vichwa vya nyuklia vinavyoweza kutumiwa vitani. Hayo yamo katika ripoti mpya ya shirika linalochunguza biashara ya silaha, SIPRI.

Russland Atomwaffen
Picha: picture-alliance/AP Photo/Russian Television

Kwa mujibu wa shirika hilo lenye makao yake nchini Sweden, nchi 9 duniani zinazo silaha za nyuklia, zikiongozwa na Urusi na Marekani. Nchi nyingine ni China, Uingereza, Ufaransa, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini.

Ripoti ya SIPRI inasema kwa pamoja nchi hizo zina vichwa vya nyuklia 13,865 mwaka huu wa 2019, vikijumuishwa vile ambavyo havijaunganishwa kwenye makombora, na vilivyo kwenye orodha ya kukongolewa.

Soma zaidi: SIPRI: Bado Silaha za nyuklia zinatengezwa

Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ya mwaka 2018, ambapo nchi hizo zilikuwa na jumla ya vichwa 13,925.

Hiyo inamaanisha kuwa vichwa 600 vya nyuklia vilikongolewa, mchakato huo ukiongozwa na Urusi na Marekani chini ya makubaliano yajulikanayo kama START mpya.

Urusi na Marekani zaongoza kwa shehena ya nyuklia

Urusi inavyo vichwa vya nyuklia 6,500 na inafuatiwa na Marekani yenye vichwa vya 6,185 vya silaha hizo. Robo ya silaha hizo ziko katika utayarifu wa mashambulizi wakati wowote.

Makubaliano ya START mpya yalisainiwa na marais wa zamani, Barack Obama wa Marekani (kushoto) na Dmitry Medvedev wa UrusiPicha: picture-alliance/dpa/S. Chirikov

Katika nafasi ya tatu inakuja Ufaransa iliyo na vichwa vya namna hiyo 300, ikifuatiwa kwa karibu na China ambayo inavyo 290. Uingereza inavyo 200, Pakistan 160, India 140, nayo Israel inavyo vichwa vya nyuklia vipatavyo 90.

Lakini mchakato huo wa kupunguza zana za kinyuklia hautarajiwi kuendelea baada ya mwaka 2021 ambao ni mwisho wa mkataba wa START mpya baina ya Urusi na Marekani, kwa sababu hakuna mazungumzo yoyote yanayofanyika kwa nia ya kuurefusha.

Soma zaidi: SIPRI na tathmini ya machafuko arabuni 

Mkuu wa kitengo cha kuangamizwa kwa silaha za nyuklia na udhibiti dhidi ya kusambaa kiholela kwa silaha katika shirika la SIPRI Shannon Kile amesema ''hali ya mvutano na uhasama baina ya nchi hizo kwa wakati huu haileti matumaini kuwa mazungumzo hayo yataanzishwa hivi karibuni''.

India na Pakistan katika mashindano

Silaha za nyuklia za Pakistan katika maonyesho ya kitaifaPicha: Getty Images/AFP/F. Naeem

Kile ametahadharisha kuwa India na Pakistan ziko mbioni kuongeza uwezo wao wa kinyuklia katika kiwango ambacho kinaweza kuzidisha mlundikano wa silaha za nyuklia duniani mnamo muongo mmoja ujao.

Shirika la SIPRI limekadiria kuwa Korea Kaskazini inavyo vichwa vya nyuklia kati ya 20 na 30, ambavyo linaamini nchi hiyo inavichukulia kama kipaumbele kwa mkakati wake wa usalama wa taifa.

Shirika hilo limesema Korea Kaskazini haijafanya majaribio yoyote ya silaha zake za nyuklia tangu ilipoingia katika mazungumzo na Marekani, kuhusu uwezekano wa kuziondoa silaha hizo.

Shannon Kile amesema kujizuia huko kunatoa ishara njema, ingawa haijulikana kutaendelea kwa muda gani, na amezihimiza Korea Kaskazini na Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

 

dpae

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW