1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Nchi zinazotambua likizo ya hedhi kwa wanawake

Sylvia Mwehozi
27 Mei 2022

Mei 28 kila mwaka ni siku ya hedhi duniani. Pamoja na changamoto nyingine wanawake wengi hupatwa na maumivu makali wakati wa hedhi, lakini ni nchi chache tu ulimwenguni ambazo zimeidhinisha ruhusa ya hedhi.

Menstruation | Produkte
Picha: Colourbox

Siku ya hedhi duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 28 ya mwezi Mei. Uhispania imekuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kuelekea kutoa likizo ya hedhi kwa wanawake. Rasimu ya muswada huo iliyowasilishwa mapema mwezi Mei, inawapatia wanawake likizo isiyo na ukomo ya maumivu ya hedhi, alimradi wawe na maelezo ya daktari.Hedhi salama bado ni changamoto kwa wasichana wa Kenya

Muswada huo utapaswa kupitishwa na bunge, kabla ya kuanza kutumiwa. Mapendekezo hayo yametolewa katikati mwa kampeni ya wanaharakati duniani kote wanaotaka kuvunjwa kwa miiko inayozunguka suala la hedhi, lakini wamekabiliwa na ukosoaji kutoka chama cha wafanyakazi cha Uhispania. Hoja yao ni kwamba hata kama ni suala la kumkomboa mwanamke, lakini likizo ya hedhi inaweza kuchochea waajiri kuwapa kipaumbele zaidi wanaume wakati wa kuajiri kuliko wanawake.

Baadhi ya wanawake na wasichana hukabiliwa na maumivu makaliPicha: Colourbox/Motortion

Indonesia ilipitisha sheria mwaka 2003 inayowapatia haki wanawake ya siku mbili za malipo ya likizo ya hedhi kwa mwezi bila ya kutoa taarifa ya awali.  Lakini utekelezwaji wake ni wa hiari. Waajiri wengi huruhusu angalau siku moja tu kwa mwezi, wakati wengine wakiwa hawana likizo ya namna hiyo kabisa, ama kwasababu ya kutofahamu sheria au kwa kupuuza tu.

Ripoti ya Shirika la kazi la kimataifa ILO ya mwaka 2003 ilionya kwamba masharti ya kupatia mwanamke siku 24 za likizo ya hedhi kwa mwaka kunatoa "gharama kubwa" kwa waajiri wengi na kusababisha ubaguzi katika mchakato wa ajira.

Nchini Japan sheria ya mwaka 1947 inatamka wazi kwamba kampuni zinapaswa kukubaliana kuwapatia wanawake likizo ya hedhi, kadri watakavyohitaji. Hata hivyo, haiwalazimishi kuwalipa wanawake wakati wa likizo hiyo, lakini karibu asilimia 30 ya makampuni ya Japan hutoa malipo kamili au sehemu tu kulingana na takwimu za wizara ya kazi.

Upatikanaji wa Sodo bado changamoto kwa wasichana na wanawake wengiPicha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Nchini Korea Kusini, wanawake wamepewa siku moja isiyo na malipo ya likizo ya hedhi kwa mwezi, huku waajiri wanaopuuza hukabiliwa na faini ya dola karibu 4,000. Likizo hiyo ilikuwa na malipo hadi kufikia mwaka 2004 wakati Korea Kusini ilipoacha kufanya kazi siku sita kwa wiki hadi tano.

Huko Taiwan, sheria ya usawa wa kijinsia na ajira huwapatia wanawake siku tatu za likizo ya hedhi kwa mwaka. Kama ilivyo kwa likizo ya kuumwa, wafanyakazi wanaochukua likizo ya hedhi hulipwa asilimia 50 ya mshahara.

Mnamo mwaka 2015, Zambia ilikuwa miongoni mwa nchi nyingine za Kiafrika kupitisha sheria inayowaruhusu wanawake kukaa nyumbani siku moja wakati wa hedhi, bila kutoa taarifa au kutoa barua ya daktari. Ingawa hatua hiyo inakubaliwa na kuungwa mkono kwa ujumla, si waajiri wote wanaotii sheria kwa hiari kuhusu kile kinachojulikana kama "Siku ya akina mama".

Mwanadada aliyetengeneza Hedhi App inayotoa msaada kwa wanawake

03:34

This browser does not support the video element.

Wakiungwa mkono na vyama vya wafanyakazi, wanawake wameanza kutumia haki yao, anasema mtaalamu wa mawasiliano na mwanaharakati wa haki za wanawake Ruth Kanyanga kama alivyozungumza na shirika la habari la AFP.

Baadhi ya kampuni hazikungoja kushurutishwa na sheria ili kuwapatia wanawake likizo ya hedhi. Baaadhi ya kampuni  hizo ni ile ya Australia ya Victoria Women's Trust ambayo huwapa wafanyakazi siku 12 za likizo ya hedhi na kukoma hedhi.

Kampuni nyingine ya huko India ya Zomato, nayo imetoa siku 10 za likizo ya kipindi cha hedhi. Nyingine ni ya Ufaransa ya French La Collective, ambayo inatoa siku moja ya likizo ya hedhi kwa mwezi.