1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zipi duniani zinaongoza kwa idadi ya wabunge wanawake?

14 Februari 2023

Kulingana na data kutoka katika Muungano wa Mabunge Kimataifa unaofuatilia IPU, zipo nchi sita duniani ambazo idadi ya wabunge wanawake ni nusu ya idadi jumla ya wabunge wote.

Schweiz Genf 2018 | Inter-Parliamentary Union
Picha: Utku Ucrak/Anadolu Agency/picture alliance

Kulingana na Muungano wa Mabunge Kimataifa IPU, kuna zaidi ya mbunge mmoja miongoni mwa wanne ulimwenguni. Hiyo ni tofauti na hali ilivyokuwa mwaka 2011, ambapo ungempata mbunge mwanamke mmoja tu miongoni mwa wabunge watano.

Kwa mujibu wa IPU, kuanzishwa kwa vitengo maalum vya kijinsia ni sehemu ya mafanikio hayo katika miaka ya hivi karibuni.

Zaidi ya theluthi mbili ya nchi ulimwenguni ambazo zimepita asilimia 40 ya uwakilishi wa wanawake bungeni, zina baadhi ya vitengo au viti maalum kwa wanawake.

Lakini nchi nyingine hazijakuwa na mabadiliko yoyote chanya. Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya wanawake, juhudi za kuziba ukosefu wa usawa kijinsia katika uwakilishi bungeni hazitafanikiwa kabla ya mwaka 2063.

Hali halisi ya idadi ya wanawake wabunge

Rais Paul Kagame wa Rwanda akisimama na wabunge wapya waliochaguliwa mwaka 2018 nje ya majengo ya bunge mjini Kigali Septemba 19, 2018.Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Je ni nchi zipi zimepiga hatua mbele, na ni zipi zimerudi nyuma katika kufanikisha usawa wa kijinsia kati ya idadi ya wanawake na wanaume bungeni?

Kulingana na data kutoka Muungano wa Mabunge IPU, zipo nchi sita ambazo idadi ya wabunge wanawake ni nusu ya wabunge wote.

Nchini Rwanda, zaidi ya asilimia 60 ya viti bungeni ni wanawake. Hali hiyo iliifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza ulimwenguni kuwa na bunge lenye wanawake wajumbe wengi zaidi ulimwenguni mwaka 2008.

Nchini Cuba, idadi ya wabunge wanawake pia imeshinda idadi ya wabunge wanaume kwa wastani wa 53:52.

New Zealand, Mexico na Umoja wa Falme za Kiarabu zote zina idadi sawa ya wabunge wanaume na wanawake bungeni, huku Iceland, Costa Rica, Sweden na Afrika Kusini pia zikitajwa kuwa na uwakilishi usio mbaya wa wabunge wanawake bungeni.

Idadi ya wabunge wanawake Tunisia kupungua

Idadi ya wabunge wanawake nchini Tunisia inatarajiwa kushuka baada ya uchaguzi wa hivi karibuni katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika ambalo tangu zamani limekuwa likiongoza katika haki za wanawake katika kanda hiyo.

Matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanywa Disemba na Januari nchini humo, yanaashiria kwamba wanawake watashinda asilimia 16 pekee ya viti, kwa mujibu shirika lisilo la serikali la Femmes et Leadership.

Asilimia hiyo ni ya chini ikilinganishwa na asilimia 26 ya viti mwaka 2021 na asilimia 31 ya uwakilishi wa wanawake bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Lakini licha ya hayo, hali nchini Tunisia inasalia kuwa tofauti na hali jumla ulimwenguni.

Yemen yashika mkia kuhusu idadi ya wanawake bungeni

Yemen ni miongoni mwa mataifa yanayoshika mkia kuhusu idadi ndogo ya wajumbe wanawake bungeni. Katika bunge la Yemen, hakuna hata mbunge mmoja mwanamke. Nayo nchi ya Vanuatu, ina mbunge mmoja pekee mwanamke.

Nchini Afghanistan, kundi la Taliban limewazuia wanawake kushiriki kazi za hadharani, tangu lilipochukua madaraka mwaka 2021.

Kabla yahapo, wanawake walishikilia asilimia 27 ya viti katika bunge lisilofanya kazi sasa. Wengi wa waliokuwa wabunge wanawake wameikimbia nchi hiyo.

Katika zaidi ya nchi 20, wanawake wanashikilia asilimia 10 ya uwakilishi bungeni, ikiwemo Nigeria iliyo na asilimia 3.6, Qatar ikiwa na asilimia 4.4 na Iran iliyo na asilimia 5.6.

Idadi ya wabunge wanawake nchini Tunisia inatarajiwa kupungua baada ya uchaguzi uliopita mwezi Disemba.Picha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Sri Lanka iliweka historia ya kuwa na mwanamke wa kwanza Waziri Mkuu

Sri Lanka ambayo iliwahi kuwa na waziri mkuu wa kwanza mwanamke  mnamo mwaka 1960, ni miongoni mwa nchi zinazojikokota. Katika miaka 25 iliyopita, idadi ya wanawake bungeni nchini humo imekuwa takriban asilimia 5.

Miongoni mwa nchi zilizo na nguvu kiuchumi, Japan inashika mkia ikiwa na asilimia 10 pekee ya wabunge wanawake.

Ulimwenguni kote, ni moja juu ya tano pekee ya mawaziri ni wanawake na mara nyingi wanapewa wizara zinazohusiana na afya, familia, masuala ya jamii na mazingira.

Nchi ambazo zimewateua wanawake wengi kwenye mabaraza yao ya serikali ni pamoja na Uhispoania, Albania, Colombia na Rwanda.

Algeria na Tunisia ni kati ya nchi ambazo zimerudi nyuma sana ulimwenguni.

Mnamo mwaka 2021, idadi ya wanawake nchini Algeria ilishuka kutoka asilimia 26 hadi 8% kufuatia mageuzi kwenye mifungo ya vitengo vya uwakilishi.

Mhariri: Mohammed Khelef