Mkwamo wa kisiasa nchini Haiti waelekea mwisho
20 Julai 2021Wahaiti wameanza msururu wa sherehe kadhaa rasmi leo za kumuenzi rais Jovenel Moise aliyeuwawa nyumbani kwake wiki mbili zilizopita.
Mwili wa rais wa Haiti aliyeuwawa ulitarajiwa kupelekwa ikulu kabla ya alfajiri katika makumbusho ya kitaifa ya Pantheon kwenye mji mkuu wa Port-au Prince,ikiwa ni mwanzo wa sherehe za kumuenzi na kutoa heshima ya mwisho kwa kiongozi huyo aliyeuwawa Julai 7 baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake na mkewe kujeruhiwa vibaya.
Sherehe hizi zinafanyika katika wakati ambapo waziri mkuu mteule Ariel Henry anajiandaa kumrithi waziri mkuu wa mpito Claude Joseph aliyechukua uongozi wa Haiti baada ya mauaji ya rais Moise akisaidiwa na polisi na jeshi la nchi hiyo.Haijafahamika ni wakati gani Henry ataapishwa lakini katika ujumbe wa sauti ameahidi kwamba hivi karibuni atatangaza ni nani ataunda serikali ya mpito ya maridhiano itakayoiongoza nchi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu.
Mabadiliko haya ya uongozi nchini Haiti yanakuja baada ya kundi la wanadiplomasia muhimu wa kimataifa likiwajumuisha mabalozi wa Ujerumani,Brazil,Canada,Uhispania,Marekani,Ufaransa na Umoja wa Ulaya pamoja na wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Amerika kutoka kutaka Henry aunde serikali ya maridhiano ya Umoja wa kitaiafa.
Waziri anayehusika na masuala ya uchaguzi Mathias Pierre jana aliwaambia wandishi habari kwamba waziri mkuu Joseph ataachia ngazi na kumpisha Arial Henry aliyeteuliwa kuchukua nafasi hiyo na rais Moise kabla ya kuuwawa. Robert Fatton mtaalamu wa siasa za Haiti kutoka chuo kikuu cha Virginia anasema Kuondoka kwa Joseph madarakani ni kitu kilichotarajiwa na kila kitu kinachoendelea Haiti kina ridhaa ya nchi za kigeni zenye nguvu.
Jana Umoja wa Mataifa ulisema kwamba Joseph na Henry wamepiga hatua kwenye mazungumzo ya kumaliza mkwamo na kwamba unaunga mkono mazungumzo ya kutafuta maridhiano ya kufanyika uchaguzi wa huru na wa haki wa bunge na rais nchini humo.
Kimsingi ni kwamba hakutokuwa na rais wa Jamhuri nchini Haiti kwa sasa na serikali mpya itakayoongozwa na Arial Henry kama waziri mkuu itawajibika kuandaa uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo. Joseph aliyejipa uwaziri mkuu atarudi kwenye nafasi yake ya zamani ya waziri wa mambo ya nje katika serikali hiyo mpya.Marekani imeipongeza hatua hiyo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba