1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maeneo yanayohofiwa kukumbwa na ghasia za uchaguzi Kenya

Admin.WagnerD1 Juni 2022

Majimbo sita nchini Kenya yametajwa kuwa na viwango vya juu vya kushuhudia ghasia za uchaguzi mkuu ujao kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Uwiano na Utangamano-NCIC.

Kenia Wahlen Unruhen Demonstration der Opposition in Kisumu
Picha: AP

Utafiti huo wa NCIC umefanywa ili kufahamu hali halisi ya usalama na kuweka mikakati inayostahili kuzuia ghasia. Ripoti hiyo inaliweka eneo la Nairobi katika nafasi ya kwanza ikiwa na asilimia 79 ikifuatiwa na majimbo ya Nakuru, Kericho, Kisumu, Uasin Gishu na Mombasa. Kwenye chaguzi za awali majimbo hayo, yaliwahi kushuhudia machafuko ambapo watu kadhaa waliuwawa, wengine kujeruhiwa na hata makazi kuteketezwa. Ripoti hiyo inataja idadi kubwa ya watu katika mitaa ya mabanda, ugavi wa raslimali na magenge kuwa baadhi ya sababu zinazoleta machafuko.  Kasisi Samwel Kobia ni mwenyekiti wa Tume ya Uwiano na Utangamano. Katika historia ya taifa la Kenya, miezi michache kabla ya uchaguzi kufanyika, machafuko hushuhudiwa. Kobia alifichua kuwa tayari wanachunguza visa 49 vya matamshi ya kuchochea  chuki.

Mipango ya kuanzisha kesi za kukabiliana na uchochezi yaendelezwa

Mipango Iko mbioni kuanzisha korti nne kote nchini za kukabiliana na wachochezi. Hata hivyo, hakuna mwanasiasa aliyewahi kuhukumiwa kwa sababu ya uchochezi, wadadisi wakisema kuwa tume hiyo haina meno ya kung'ata kwenye utendajikazi wake. Jaji Mkuu Martha Koome ameteua mahakimu 119 kusikiliza na kuamua kesi zinazohusiana na uchaguzi. Ripoti hiyo pia imesema, polisi huenda wakalazimika kutumia nguvu kupita kiasi, hali ambayo itavuruga amani. Majukwaa ya mitandao ya kijamii pia yametajwa kuwa vyanzo vya machafuko kwa wachochezi.

Wambui Nyutu, naibu wenyekiti wa Tume ya NCIC amesema kuwa ripoti hiyo itatoa dira ya jinsi maafisa wa usalama watakavyofanya kazi ya kudumisha amani.

Maeneo yaliotajawa

Ripoti hiyo inataja majimbo kumi yenye viwango vya wastani vya kushuhudiwa machafuko, huku mengine 31 yakitajwa kuwa salama. Majimbo hayo yenye viwango vya wastani ni pamoja na  Bomet, Samburu, Nandi, Meru, Isiolo, Baringo, Lamu, Laikipia, Marsabit na Narok. Aidha ripoti hiyo inataja kuwa matumizi ya dawa za kulevya huenda yakachangia machafuko kwenye uchaguzi. Takriban watu 1,200 waliuawa huku wengine 600,000 wakipoteza makazi kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka 2007. Baadhi ya mapendekezo kwenye ripoti hiyo ni kwa asasi zinazohusika na uchaguzi kama vile Idara ya Mahakama na Tume ya Kusimamia Uchaguzi ziendeshe majukumu yao bila ya kuingiliwa na hatimaye zifanya maamuzi huru na ya haki, kutatua mizozo kwenye mipaka inayoshuhudia wizi wa mifugo na kuendelea kuuhamasisha ummaa. Zimesalia siku 68 kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW