1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndayishimiye ziarani Kinshasa kujadili amani, ushirikiano

28 Agosti 2023

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi yuko mjini Kinshasa kujadili masuala ya maslahi ya pamoja kati ya pande hizo mbili wiki chache baada ya mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioafanyika Bujumbura.

Kongo | Besuch des Präsidenten Burundis Evariste Ndayishimiye bei Felix Tshisekedi
Picha: Giscard Kusema

Miongoni mwa masuali ambayo Felix Tshisekedi na Evariste Ndayishimiye waliyagusia ni pamoja na amani, uhusiano na biashara.

Marais hao wawili walisikitishwa na kitendo cha kukosekana nia kwa upande wa waasi wa M23 kujiondoa katika maeneo wanayoyadhibiti mkoani Kivu Kaskazin na wakatowa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwalazimisha waasi hao kuondoka.

"Tunatambua kwamba vikundi vingine vinavyomiliki silaha Kongo vimekubali kuweka silaha chini, lakini M23 bado hawajakubali. Kwa hiyo, tunaomba sote tuungane ili kuwalazimisha kusitisha vita na kuyaacha maeneo wanayoyadhibiti. Msimamo wetu ni kwamba Kongo lazima iwe tena na amani." Alisema Ndayishimiye, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa EAC.

Mkutano wa kilele wa jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika hivi karibuni na ni katika mkutano huo ndipo marais watashughulikia suala hilo.

 DRC kuchunguza ahadi za M23

Lakini kabla ya hayo, Rais Tshisekedi alisema serikali yake itaendelea kuchunguza kama M23 hatimaye itaheshimu ramani ya EAC.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amefanya mazungumzo na mwenzake wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.Picha: Giscard Kusema

Soma zaidi: Rais Tshisekedi kukutana na viongozi wa waasi wa Kongo

"Kama sivyo, yaani wasipoheshimu, tutapata matokeo katika mkutano wa hivi karibuni. Lakini mahitaji yetu yanabaki yale yale. Yaani tunaomba vikosi vya kikanda kutumika kama vile kikosi cha Burundi kinavyofanya kwani katika baadhi ya maeneo tunaendelea kuona ulegevu." Alisema Tshisekedi.

Ulegevu huo ndio uliotajwa pia na Jean-Claude Bambaze, kiongozi wa shirika la kiraia la Rutshuru, mojawapo ya maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa waasi, ambaye aliiambia DW kwamba licha kuwepo kikosi cha EAC, bado hali ya usalama inazidi kuzorota.

"Sisi hatujaona kazi au msaada wa EAC kwa sababu badala ya kuwasaka hawa wanamgambo wa M23, leo wamekuwa marafiki zao wakikaa pamoja na kuchangia pombe. Hii inamaanisha kuwa wao na EAC ni watu wamoja tu." Alisema mwanaharakati huyo.

Kwa upande mwengine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi zimesaini makubaliano ya kijeshi katika mfumo wa ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi hizo mbili.

Imeandaliwa na Jean Noel Ba-Mweze/DW Kinshasa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW