1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege wasababisha hasara kwenye mashamba ya mpunga Kisumu

17 Januari 2023

Wakulima wa mpunga jimboni Kisumu eneo la Nyanza Magharibi mwa Kenya wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa baada ya ndege kuvania mazao yao

Blutschnabelweber - Red billed Quelea
Picha: picture alliance/Bildagentur-online

Uvamizi wa ndege aina ya nyuni katika mashamba ya mpunga ya kunyunyizia maji ya Kano Magharibi, jimboni Kisumu umewaacha wakulima wa zao hilo na hasara ya takriban zaidi ya shilingi milioni 20 ikikadiriwa kuwa, hasara zaidi itaendelea kushuhudiwa endapo hatua za dharura hazitachukuliwa kuwadhibiti ndege hao ambao inadaiwa wanakula chakula mara mbili ya uzani wao kila siku.

Wakulima hao ambao wamelazimika kuraukia mapema mashambani na kuondoka majira ya machweo wanasema, juhudi za kuwafukuza ndege hao kwa kelele nyingi na matumizi ya vinyago mashambani zimegonga mwamba baadhi yao wakisusia kilimo cha mpunga kutokana na hasara ya uvamizi wa mara kwa mara wa ndege hao.

Kilio cha wakulima hao wa eneo la Nyando kimesikika huku wizara ya kilimo ikianza mpango wa kunyunyiza kemikali ya kuwadhibiti ndege hao ambao imeelezwa kuwa, idadi yao Nyando imefika takriban milioni 10.

Waziri wa kilimo jimbo la Kisumu Ken Onyango anasema nyuni hao wameharibu mpunga katika hekari 300 za mashamba eneo hilo huku pakiwa na mpango zaidi wa unyunyizaji huo utakaolenga maeneo mengine kama Muhoroni, Alara, Ogange, unyunyiziaji huo ukiidhinishwa na kitengo cha ukuzi wa mimea na utafiti.

Hata hivyo, hatua hii imeonekana kupata pingamizi nzito kutoka kwa wanaharakati wanaotetea maslahi ya mazingira wanaosema unyunyiziaji huo wa kemikali utakuwa na athari kubwa kwa ndege, wadudu, wanadamu na mazingira jumla ya sehemu hiyo.

Tom Ogolla mwanaharakati wa mazingira kutoka shirika la Jijenga Youth Organization anasema ni muhimu kwa wizara husika kutafakari hatua hiyo ikizingatiwa atahari yake ambayo anasema mwisho wake ni hadi Ziwani Victoria ambapo maji kutoka mashamba hayo kupitia mikondo ya maji itaelekezwa Ziwani sawia na ndege watakaokufa na pia athiri ya kemikali kwa odongo mashamba humo.

Ogolla ameshikilia kuwa, ni muhimu kutumiwa kwa mbinu kama zinnazotumiwa katika mataifa mengine kama vile kuwafukuza kwa kupiga makelele na kuekeza katika utafiti zaidi kutafuta mbinu zaidi za kuwadhibiti ndege hao.

Mwandishi: Mussa Naviye/DW Kisumu
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW