1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NDEGE YA ABIRIA YAANGUKA NIGERIA

23 Oktoba 2005

TAARIFA YA HABARI 23-10-05 12.00

Ndege ya abiria iliopakia hadi watu 114 imeanguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka Lagos ikielekea Abuja,mji mkuu wa Nigeria.Ndege hiyo chapa Boeing 737 ilitoweka katika mtambo wa rada kwa zaidi ya masaa 8 na wakuu waliarifu kuwa,yamkini imejitosa katika bahari ya Atlantik.Mashahidi 2 waliripoti kujionea kitu kikubwa kikijibwaga baharini.

Inaaminiwa kuwa, ndani ya ndege hiyo mlikuwamo waheshimiwa kadhaa wa kingieria .Ndege za helikopta zinawasaka waliookoka na maisha .Ndege hiyo -mali ya shirika la kibinafsi la Bellview iliruka mnamo saa 1.50 za jioni jana -saa za Nigeria ikielekea Abuja.

MEXICO:

Kimbunga kikali ‚WILMA’ kiliendelea kuutikisa mwambao wa pwani ya karibik wa Mexico kwa siku ya pili jana na kun’goa mapaa ya majumba,milango ya maduka na kuwalazimisha watalii na wakaazi kuparamia na kujikusanya ghorofa za juu za majumba.Si chini ya watu 7 wameuwawa.

Wataalamu wa utabiri wa hali ya hewa wanasema kimbunga wimla sasa kimepungua kasi na kufikia kipimo cha 2 lakini kinatarajiwa kupata tena nguvu kielekea mkoa wa Florida,Marekani.

Mbali na hayo, kimbunga cha 22 –rekodi kwa jina la Alpha kinavuma katika pwani ya kisiwa cha Hispanola baina ya haiti na Jamhuri ya Dominika.

KABUL:

Mtetemeko wa ardhi unaripotiwa umezuka mashariki mwa Afghanistan karibu na mpaka na Pakistan.Si chini ya watu 5 wameuwawa na wengine 6 wamejeruhiwa.Taarifa za kwanza pia zinasema kuwa, baadhi ya majumba yameporomoka katika zilzala hiyo iliozuka katika mkoa wa Paktika.

Wakuu wamearifu timu za uokozi za wanajeshi zikielekea huko sehemu za milimani .Zilzala nyengine ilipiga mpakani na mkoa Zabul-unaopakana na mkoa wa Paktika.

NEWDELHI

India imejitolea kuunda kambi za misaada ya uokozi upande wake wa eneo la Kashmir ili kutoa hoduma kwa waliofikwa na maafa ya zilzala .Hatua hii imefuatia mwito aliotoa rais Pervez Musharraf wa Pakistan, alipotaka wakashmiri wote kuruhusiwa kuvuka mpaka wa kusimamisha mapigano ili kusaidiana kwa maafa yaliotokea.Pakistan imearifu hatahivyo, kuwa m ajadiliano zaidi yanahitajika juu ya pendekezo hilo .Hatahivyo, unanabainisha dalili ya utayarifuwa unaozidi wa kushirikiana kati ya mahasimu hawa wawili wenye silaha za kinuklia.

Hadi watu 80.000 wanakisiwa wamefariki katika mtetemeko wa ardhi uliopiga hapo Oktoba 8 na hasa upande wa kaskazini mwa Pakistan.

STOCKHOLM:

Sweden imethibitisha kesi moja ya homa ya ndege iliothiri bata waliokutikana wamekufa magharibi mwa mji mkuu Stockholm.Wakuu wa Idara ya siha hatahivyo, wamesema bado hawajui kwa uhakika,iwapo maradhi hayo yangeweza pia kuwaambukiza binadamu.Maradhi ya homa ya mafua ya ndege yamegunduliwa nchini Russia,Uturuki,Romania na Croatia hivi karibuni.Yameua watu 61 katika nchi mbali mbali za Asia.

Ujerumani imeamrisha mifugo yote ya aina ya kuku na bata kubakia ndani katika juhudi za kuzuwia kutapakaa kwa maradhi hayo.

ARBIL:

Katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League-Amr Mussa, ameitisha pawepo na Iraq mpya alipohutubia Bunge la wakurdi hii leo wakati wa ziara ya kihistoria yenye shabaha ya kupalilia mkutano wa kuleta umoja wa taifa la Irak.

Amr Mussa anaeongoza Jumuiya ya nchi za kiarabu ya wanachama 22, aliwasili jana Arbil,kwa wakurdi na kukutana na rais wa mkoa huo Massoud Barzani katika ziara inayobainisha kunyosha mkono wa suluhu wa Arab League kwa eneo hilo la wakurdi lenye mamlaka yake ya ndani.

JERUSELEM:

Wapalestina 16 miongoni mwao wafuasi 13 wa HAMAS wametiwa nguvuni jana usiku huko ukingo wa magharibi .Wote walikamatwa huko Hebron ikiwa sehemu ya wimbi la kamata-kamata kufuatia jaribio la wapalestina lililoshindwa la ufyatuaji risasi wiki iliopita.

Wapalestina 15 pia walikamatwa usiku uliotangulia wa jana wakati wa msako wa usiku kuongoza kugunduliwa bomu la mkono lililofichwa chini ya blanketi la mtoto mchanga.

STRASBOURG:

Bunge la Ulaya litajadili kesho mipango ya kuregeza sheria inayopangwa kutungwa juu ya kukusanya na kuhifadhi taarifa za watu wanaoshukiwa ugaidi ambayo Uingereza na wanachama wengine wa UU zinataka kuipitisha hadi mwisho wa mwaka huu.

Serikali za UU ziliafikiana mapema mwezi huu kuzitaka kampuni za mawasiliano ya simu kuhifadhi rekodi za simu watu walizopiga alao kwa mwaka na barua pepe kwa alao miezi 6 ikiwa sehemu ya kampeni hiyo.

Uingereza, mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, inapendelea sheria kali za kupambana na ugaidi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW