Ndege ya kijeshi ya Urusi yaanguka na kuua watu wote 74
24 Januari 2024Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA limeripoti kuwa ndani ya ndege hiyo walikuwemo wafungwa wa kivita 65 wa Ukraine waliokuwa wakisafirishwa kwenda Belgorod, wafanyakazi sita wa ndege hiyo, pamoja na wasindikizaji watatu.
Gavana wa jimbo la Belgorod, Vyacheslav Gladkov, amesema watu wote waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wamekufa. Ikulu ya Urusi ya Kremlin imesema inalichunguza tukio hilo.
Ndege hiyo ya kijeshi aina ya Ilyushin chapa II-76 imetengenezwa kwa ajili ya kubeba wanajeshi, mizigo na vifaa vya kijeshi. Kwa kawaida huwa ina wafanyakazi watano na inaweza kubeba hadi abiria 90.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imevishutumu vikosi vya Ukraine kuwa vimeidungua kwa makusudi ndege hiyo, na kukiita kitendo hicho kuwa cha ''kigaidi'' na ''kishenzi''.
Ndege imedunguliwa kwa makombora kutoka Ujerumani au Marekani
Mbunge wa Urusi na mjumbe wa kamati ya ulinzi ya bunge, Andrei Kartapolov, amesema kuwa ndege hiyo imedunguliwa kwa makombora ya Marekani au Ujerumani yaliyotolewa kwa Ukraine. ''Ndege ya kijeshi iliyoanguka Belgorod, imedunguliwa kwa makombora matatu chapa Patriot, au mfumo wa ulinzi wa anga chapa Iris-T, ambayo mataifa ya Magahribi yameipatia Ukraine,'' alifafanua Kartapolov.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi, wataalamu wa rada ya Urusi wamegundua kuwa makombora mawili ya Ukraine yalirushwa kutoka kwenye jimbo la Kharkiv, eneo linalopakana na Belgorod, wakati ndege hiyo ilipodunguliwa. Hata hivyo, wizara hiyo haijatoa ushahidi wowote kuhusu madai hayo.
Soma zaidi: Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa
Urusi imesema kuwa uongozi wa Ukraine ulikuwa unafahamu kwamba kulingana na utaratibu uliowekwa, wanajeshi wa Ukraine watasafirishwa kwa ndege ya kijeshi kwenda uwanja wa ndege wa kijeshi wa Belgorod ili kubadilishana wafungwa.
Taarifa hiyo imesema kulingana na makubaliano ya awali tukio hilo lilikuwa lifanyike majira ya mchana kwenye kituo cha ukaguzi cha Kolotilovka kilichoko kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine.
Urusi: Ajali hiyo ni hujuma
Gladkov amesema tukio hilo limefanywa kuhujumu zoezi la kubadilishana wafungwa. Amesema ndege ya pili ya Urusi chapa II-76 iliyokuwa na wanajeshi wapatao 80 wa Ukraine waliokuwa wabadilishwe ilifanikiwa kugeuka na kurudi ilikotoka.
Mykhailo Podolyak, mshauri wa rais wa Ukraine ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watazungumza baadaye kuhusu tukio hilo, na kwamba wanahitaji muda kuthibitisha taarifa zote. Awali, maafisa wa Kiev walionywa dhidi ya kutoa taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Katika hatua nyingine, msemaji wa serikali Ujerumani amesema kuwa upelekwaji wa silaha za ziada nchini Ukraine, kusaidia katika mapambano yake na Urusi, itakuwa ajenda ya kujadiliwa wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo, mjini Brussels.
(AP, DPA, Reuters)