Ndege ya kivita ya Marekani yadunguliwa Iran
4 Aprili 2026
Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vimeingia hatua mpya ya hatari baada ya ripoti kueleza kuwa ndege mbili za kijeshi za Marekani zimeanguka katika siku moja ndani na karibu na eneo la Ghuba.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, ndege ya kwanza aina ya F-15E Strike Eagle ilidunguliwa juu ya ardhi ya Iran, huku ndege ya pili aina ya A-10 Warthog nayo ikiripotiwa kuanguka katika eneo la Ghuba, karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
Taarifa za awali zilisema mhudumu mmoja wa ndege ya F-15E aliokolewa akiwa hai, wakati operesheni ya kumtafuta mhudumu mwingine iliendelea chini ya mazingira hatari ya kivita.
Ndege ya A-10 Warthog, ambayo awali ilitajwa kutumiwa kushambulia meli za Iran katika Mlango wa Hormuz, iliripotiwa pia kuanguka Ijumaa, ingawa maelezo kamili ya tukio hilo hayakuwekwa wazi mara moja.
Kwa jumla, tukio hilo limeongeza wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa Iran kuathiri moja kwa moja operesheni za Marekani angani, pamoja na kuonyesha kuwa vita hii sasa imepanuka zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Operesheni ya uokoaji na taarifa za siri
Maafisa wa Marekani na Israel, waliokataa kutajwa majina yao kutokana na unyeti wa operesheni hiyo, walieleza kuwa uokoaji wa mhudumu mmoja ulifanyika wakati jeshi la Marekani likiendesha operesheni ya kutafuta manusura.
Israel ilisema kuwa inasaidia Marekani katika juhudi hizo kwa kutoa taarifa za kijasusi, ingawa haikuhusika moja kwa moja na shughuli za uokoaji ardhini.
Vyombo vya habari vya Iran vilidai kuwa jeshi lao ndilo lililoidungua ndege ya Marekani aina ya F-15E Strike Eagle, madai yaliyoongeza mvutano na kuipa Tehran nafasi ya kuonyesha mafanikio ya kijeshi dhidi ya adui yake mkubwa.
Barua pepe kutoka Pentagon iliyonukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani ilithibitisha tu kuwa jeshi lilipokea taarifa ya "ndege kupigwa” Mashariki ya Kati, bila kufafanua zaidi aina ya ndege au mazingira kamili ya tukio.
Ikulu ya Marekani nayo ilisema Rais Donald Trump ameelezwa kuhusu tukio hilo, lakini haikutoa maelezo ya ziada kuhusu hatima ya wahudumu wote wa ndege hiyo.
Hatima ya rubani wa pili bado kitendawili
Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Bunge la Marekani iliarifiwa kuwa hali ya rubani wa pili wa F-15E bado haijulikani baada ya kuangushwa kwa ndege hiyo.
Kwa mujibu wa wasaidizi wa bunge, taarifa hiyo inamaanisha kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani haijui alipo mhudumu huyo na kwamba huenda anatambuliwa rasmi kama aliyepotea vitani.
Ripoti nyingine zilieleza kuwa , jambo linalofanya utafutaji wa mhudumu wa pili kuwa suala nyeti zaidi kwa jeshi la Marekani.
Mtaalamu wa zamani wa uchunguzi wa usalama wa Jeshi la Anga la Marekani, Alan Diehl, alisema ndege ya aina hiyo huwa na kifaa maalum cha dharura cha kutuma ishara kinachoweza kuwashwa moja kwa moja au kwa mkono.
Hata hivyo, licha ya teknolojia hiyo, operesheni ya kumtafuta mhudumu aliyepotea inaelezwa kuwa hatari sana kwa sababu ndege za uokoaji zinalazimika kuruka chini katika anga lenye uadui mkali.
Iran yaonyesha meno, Marekani yatikiswa
Mchambuzi wa kijeshi Emma Salisbury alisema tukio la kuangushwa kwa ndege ya Marekani linaonyesha wazi kuwa Iran bado ina uwezo wa kuumiza maslahi ya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Alieleza kuwa pamoja na Marekani kuwa na ndege za kisasa na zenye uwezo mkubwa zaidi kuliko Iran, droni na makombora ya Tehran bado ni tishio kubwa ambalo si rahisi kulidhibiti.
Kwa maoni yake, Marekani haina ubabe kamili wa anga juu ya Iran, na si jambo ambalo linaweza kupatikana kwa urahisi katika muda mfupi ujao.
Salisbury pia alionya kuwa ghala kubwa la droni na makombora ya Iran limeenea katika maeneo mengi ya nchi hiyo, jambo linalofanya kuwa vigumu sana kwa Marekani na Israel kuharibu uwezo huo wote kwa mashambulizi ya anga.
Kauli hiyo imezidisha mjadala kuhusu kama kampeni ya kijeshi dhidi ya Iran imepangwa vizuri au kama imeingia katika hatua ambayo gharama zake zinaweza kuwa kubwa kwa Washington na washirika wake.
Juhudi za usuluhishi zagonga mwamba
Wakati mapigano yakiendelea, juhudi za kufikia usitishaji mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran zimeripotiwa kufikia ukomo bila mafanikio.
Pakistan, ambayo iliongoza duru ya hivi karibuni ya upatanishi wa kikanda, ilikumbana na msimamo mkali kutoka Iran iliyosema haiko tayari kukutana na maafisa wa Marekani mjini Islamabad katika siku zijazo.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, Iran pia iliwajulisha wapatanishi kuwa masharti yaliyowekwa na Marekani hayakubaliki kabisa.
Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa watakubali tu kusitisha mapigano iwapo Marekani italipa fidia ya vita, itaondoa wanajeshi wake katika kambi za Mashariki ya Kati, na kutoa dhamana ya kutoishambulia Iran tena.
Katika hali hiyo, matumaini ya suluhu ya haraka ya kidiplomasia yanaonekana kufifia, huku sauti za viongozi wa kimataifa zikiendelea kupotelea katika kelele za vita.
Erdogan, Putin na wito wa kusimamisha vita
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Urusi Vladimir Putin walijadiliana kwa simu kuhusu mzozo huo na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Kwa mujibu wa Kremlin, viongozi hao walikubaliana kuwa kuendelea kwa vita kunaweza kusababisha athari kubwa zaidi kwa eneo lote la Mashariki ya Kati.
Wito huo umekuja wakati pande zinazopigana zinaonekana kuwa mbali zaidi na mazungumzo kuliko wakati mwingine wowote tangu vita hii ilipoanza.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna dalili kwamba Marekani, Israel au Iran zimebadili msimamo wao wa msingi kuhusu masharti ya kusitisha mapigano.
Hali hiyo imeongeza hofu kuwa juhudi za kimataifa za kuzuia mzozo huu kugeuka vita pana zaidi zinaweza kushindwa kabisa.
Lebanon yaingia zaidi kwenye moto wa vita
Ubalozi wa Marekani mjini Beirut umewataka raia wa Marekani kuondoka Lebanon haraka wakati safari za ndege za kibiashara bado zinapatikana.
Katika taarifa yake, ubalozi huo ulisema hali ya usalama nchini Lebanon ni tete na haitabiriki, huku mashambulizi ya anga, droni na makombora yakiripotiwa kote nchini, hasa kusini, Beqaa na baadhi ya maeneo ya Beirut.
Ubalozi huo pia ulionya kuwa Iran na makundi yake washirika yanaweza kulenga vyuo vikuu nchini Lebanon, likiwa ni onyo lililoibua hofu mpya miongoni mwa raia wa kigeni.
Onyo hilo lilitolewa wakati Israel ikiendelea na mashambulizi yake dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, hasa katika viunga vya kusini vya Beirut vinavyojulikana kuwa ngome ya Hezbollah.
Mamia ya maelfu ya wakazi tayari wameripotiwa kuyakimbia maeneo hayo, wakihofia kuendelea kwa mashambulizi makali zaidi.
Beirut na Tehran zachomwa kwa mashambulizi
Jeshi la Israel lilisema limefanya mashambulizi dhidi ya kile lilichokiita miundombinu ya ugaidi katika mji wa Beirut, huku waandishi wa habari wa kimataifa wakiripoti milipuko mikubwa katika mji huo.
Vyombo vya habari vya ndani Lebanon vilisema mashambulizi yalilenga viunga vya kusini mwa Beirut, saa chache baada ya jeshi la Israel kutoa onyo kwa raia kuhama eneo hilo.
Wakati huo huo, Israel ilisema pia imeanzisha wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya miundombinu ya utawala wa Iran katika mji mkuu wa Tehran.
Hali ya mashambulizi katika miji hiyo miwili imeonyesha wazi kuwa vita hiyo haijabaki tena kuwa ya kauli za vitisho pekee, bali imeingia katika hatua ya kushambulia maeneo ya kimkakati na ya makazi.
Mkaazi mmoja wa Tehran alisema aliona kitu kama kombora kikikatiza juu ya kichwa chake kabla ya kusikia mlipuko mkubwa na kuona moshi ukipanda karibu na eneo lenye taasisi za serikali na utafiti wa afya.
Madhara kwa raia na miundombinu yaongezeka
Mkaazi huyo wa Tehran alisema pia aliona vituo viwili vya polisi katika eneo lake vikiwa vimeharibiwa, ishara kwamba mashambulizi yanaathiri miundombinu ya kiraia na ya serikali kwa pamoja.
Katika simulizi nyingine ya maisha ya kila siku ya vita, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka arobaini alieleza kuwa kuendesha pikipiki katika mji wa Tehran kumemwonyesha sura mbili tofauti za mji huo ulio vitani.
Alisema katika maeneo tajiri ya juu ya mji, mikahawa bado ilikuwa imejaa watu ambao walitazama juu baada ya mlipuko kisha kuendelea kunywa kahawa kana kwamba hakuna kilichotokea.
Lakini katika maeneo mengine yaliyopigwa, alisema mitaa ilikuwa kimya, yenye harufu ya kifo na uharibifu, akilinganisha hali hiyo na Gaza.
Maelezo hayo yanaonyesha jinsi vita vinavyoweza kuonekana tofauti ndani ya mji mmoja, huku baadhi ya watu wakijaribu kuendelea na maisha na wengine wakizama katika hofu na majonzi.
UNIFIL yapata pigo jipya Lebanon
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, kilisema walinda amani watatu walijeruhiwa baada ya mlipuko kupiga moja ya vituo vyake kusini mwa nchi hiyo.
Wawili kati yao waliripotiwa kujeruhiwa vibaya, na wote walihamishwa hospitalini kwa matibabu ya haraka.
UNIFIL ilisema haijajua chanzo cha mlipuko huo, lakini ilizikumbusha pande zote zinazozozana kuwa zina wajibu wa kuhakikisha usalama wa walinda amani kwa kuepuka mapigano karibu na vituo vyao.
Tukio hilo lilikuwa la tatu ndani ya wiki moja, baada ya walinda amani wengine kuuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi tofauti kusini mwa Lebanon.
Kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya walinda amani kumezidisha wasiwasi kuwa vita hii sasa inahatarisha hata taasisi za kimataifa zilizowekwa kudhibiti mivutano ya mipakani.
Iran yatoa zawadi kwa marubani wa Marekani
Iran ilisema imepeleka wanajeshi na kutoa zawadi kwa yeyote atakayesaidia kukamata wahudumu wa Marekani waliodaiwa kupigwa kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la serikali la Fars lilisema vikosi vya kijeshi vimeanzisha msako wa kumtafuta rubani wa Marekani aliyepigwa mapema siku hiyo, huku raia wakitakiwa kushiriki katika utafutaji huo.
Mwandishi mmoja wa televisheni rasmi ya Iran alisema yeyote atakayewakamata marubani hao wakiwa hai na kuwakabidhi kwa polisi au jeshi atapewa tuzo kubwa.
Hatua hiyo ilitafsiriwa na wachambuzi kama sehemu ya vita vya kisaikolojia vinavyolenga kuonyesha kuwa Iran ina udhibiti juu ya eneo ilikodunguliwa ndege ya Marekani.
Wakati Iran ikiongeza msako wake, Marekani nayo iliendelea na operesheni yake ya uokoaji kwa lengo la kuwafikia manusura kabla ya wapinzani wao kufanya hivyo.
Gazeti la The Independent limemkuu Rais wa Marekani Donald Trump, akisema hawezi kuzungumzia nini Marekani itafanya ikiwa rubani huyo aliepotea atadhuriwa kwa njia yoyote na Iran.
Hormuz yaendelea kuwa kitovu cha mvutano
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliahirisha kura kuhusu pendekezo la kutumia nguvu kufungua tena Mlango wa Hormuz hadi angalau siku iliyofuata.
Pendekezo hilo, lililosukumwa na Bahrain kwa kuungwa mkono na tawala nyingine za Kiarabu za Ghuba, lingetoa ruhusa ya kutumia nguvu za "kujilinda” kulinda meli dhidi ya mashambulizi ya Iran.
Hata hivyo, rasimu hiyo ilipunguzwa makali baada ya upinzani kutoka kwa China, Ufaransa na Urusi, ambazo zote zina kura ya turufu katika Baraza la Usalama.
China ilionya kuwa kuhalalisha matumizi yasiyo ya sheria na holela ya nguvu kungeongeza zaidi hali ya mzozo na kuleta madhara makubwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, naye aliliasa Baraza hilo kuepuka kile alichokiita hatua za kichokozi zinazoweza kuuchochea zaidi mzozo huo.
Meli zaongezeka, lakini hatari bado ni kubwa
Licha ya hatari hizo, idadi ya meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz iliripotiwa kuongezeka kwa siku tatu mfululizo ndani ya wiki hiyo.
Kampuni ya data ya Windward ilisema meli 16 za mizigo zilipita Jumatano, zikilinganishwa na 11 za Jumanne, ingawa idadi hiyo bado ni ndogo sana kulinganisha na kiwango cha kabla ya vita.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa meli nyingi zilipita karibu na pwani ya Iran, hali inayoruhusu Tehran kudumisha kile kilichoelezwa kama kizuizi cha kuchagua nani apite na nani asipite.
Meli moja ya gesi asilia ya kimiminika, Sohar LNG, ilitajwa kuwa miongoni mwa meli za kwanza za aina hiyo kupita tena katika mlango huo tangu vita vilipoanza.
Wakati huo huo, Rais Donald Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii akitishia kuwa Marekani inaweza kuufungua Mlango wa Hormuz kwa nguvu, kuchukua mafuta na kupata faida kubwa, kauli iliyoongeza mshtuko na ukosoaji duniani.
Vita yatikisa uchumi na mfumo wa afya
Vita hii sasa imeingia wiki ya sita na inaendelea kuyumbisha uchumi wa dunia huku Iran ikijibu mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kulenga miundombinu ya nishati katika eneo la Ghuba.
Shinikizo juu ya usafirishaji wa mafuta na gesi kupitia Mlango wa Hormuz limeongeza hofu ya bei za nishati kupanda zaidi na kuathiri masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ametoa wito wa fedha za dharura kiasi cha dola milioni 30.3 kusaidia mifumo ya afya iliyochoka katika mataifa ya Iran, Lebanon, Iraq, Jordan na Syria.
Kwa mujibu wa WHO, mgogoro huo tayari umeua watu 3,300, kujeruhi 30,000 na kusababisha zaidi ya watu milioni nne kuhama makazi yao.
Wito huo unaonyesha kuwa mbali na medani ya vita, mgogoro huu sasa ni janga la kibinadamu linalohitaji msaada wa haraka wa kimataifa.
Kauli kali, lawama na hofu ya kesho
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, aliikejeli Marekani baada ya kuangushwa kwa ndege yake kwa kusema vita waliyoianzisha sasa imegeuka kuwa ombi la kutafuta marubani wao.
Iran pia ililishutumu Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kwa kile ilichodai ni ukimya na ushirikiano wa moja kwa moja na wanaoshambulia vituo vyake vya nyuklia.
Kwa upande mwingine, askofu mkuu Timothy Broglio, anayesimamia makasisi Wakatoliki wa jeshi la Marekani, alieleza mashaka kuhusu uhalali wa vita hiyo kwa mujibu wa nadharia ya vita vya haki.
Ndani ya Iran, baadhi ya raia wameeleza hofu kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu kunaweza kuwaacha bila umeme au maji, huku wengine wakisema wanaona maisha yao kuwa kama vifaa vya kuchezewa kati ya tawala mbili zenye nguvu.
Kadri mashambulizi, uokoaji, usuluhishi uliokwama na vitisho vipya vinavyoendelea, dunia sasa inatazama kwa wasiwasi kuona iwapo mgogoro huu utaweza kudhibitiwa, au kama unakaribia kulipuka na kuwa vita kubwa zaidi katika eneo hilo.