Ndege ya Shirika la Msalaba Mwekundu yawasili Khartoum
30 Aprili 2023Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema shehena iliyoletwa ni pamoja na vifaa vya upasuaji kwa ajili ya kuzisaidia hospitali za Sudan pamoja na wahudumu wa kujitolea wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Sudan.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, ni asilimia 16 pekee ya hospitali zinazofanya kazi katika mji mkuu Khartoum, huku vituo vingi vikiwa vimeshambuliwa katika mapigano yanayoendelea. Mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa ICRC, Patrick Youssef, amewaambia waandishi wa habari kwamba ndege iliyobeba shehena hiyo iliondoka katika mji mkuu wa Jordan, Amman na kufika katika mji wa mashariki wa Port Sudan, ambao sasa ndio mahala pekee pa kuingiza misaada kwa ajili ya watu wa Sudan.
Amesema vifaa vya matibabu kwenye ndege hiyo vinatosha kuwahudumia wagonjwa 1,500 akiongeza kuwa shirika la msalaba mwekundu linatumai litahakikishiwa usalama wa wahudumu wake ili waweze kupeleka misaada zaidi katika miji ya Khartoum na Darfur.