1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya Urusi imeanguka katika milima ya Sinai

31 Oktoba 2015

Ndege ya Urusi ikiwa na watu 224 imeanguka kwenye eneo la milima katika Rasi ya Sinai nchini Misri Jumamosi (31.10.2015) na kuuwa watu wote waliokuwemo ndani wakiwemo watoto 17´.

Ndege aina ya Airbus ya shirika la ndege la Urusi la Kogalymavia.
Ndege aina ya Airbus ya shirika la ndege la Urusi la Kogalymavia.Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Belyakova

Ndege ya Urusi ikiwa na watu 224 imeanguka kwenye eneo la milima katika Rasi ya Sinai nchini Misri Jumamosi (31.10.2015) na kuuwa watu wote waliokuwemo ndani wakiwemo watoto 17 ikiwa ni dakika 23 baada ya kuruka kutoka mji wa kitalii wa Bahari ya Sham.

Ubalozi wa Urusi umesema kupitia mtandao wake wa Facebook kwamba kwa bahati mbaya abiria wote waliokuwemo katika ndege hiyo ya shirika la ndege la Kogalymavia safari nambari 9268 kutoka Sharm el -Sheikh nchini Misri kwenda St.Petersburg nchini Urusi wamekufa.Taarifa hiyo pia imetuma rambi rambi kwa familia na marafiki waliopoteza watu wao katika ajali hiyo.Rais Vladimir wa Putin wa Urusi ametangaza Novemba Mosi kuwa siku ya maombolezo ya taifa kufuatia ajali hiyo.

Adel Mahgoub wa kampuni ya taifa ambayo inasimamia viwanja vya ndege vya kiraia nchini Misri amesema abiria 214 walikuwa ni Warusi,watatu raia wa Ukraine na wafanyakazi saba wa ndege hiyo chapa ya Airbus walikuwa ni raia wa Urusi.

Taarifa ya wizara imesema timu za uokozi za kijeshi za Misri zimeyagunduwa mabaki ya ndege hiyo ya abiria katika eneo la Hassana kusini mwa mji wa Al Arish ulioko kaskazini mwa Sinai ambapo vikosi vya usalama vya Misri vinapambana na wimbi la uasi unaozidi kuongezeka wa wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali wakiongozwa na tawi la kienyeji la Kundi la Dola la Kiislamu.

Dola la Kiislamu ladai kuhusika

Tawi hilo limedai kuidunguwa ndege hiyo katika taarifa iliyoisambaza kwenye mitandao ya kijamii.Wanamgambo hao walioko kaskazini mwa Sinai hadi sasa hawakuwahi kuidungua ndege ya abiria au ndege ya kivita.

Wanajeshi wa Misri wanaopambana na wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali kaskazini mwa Sinai.Picha: picture-alliance/dpa/Gharnousi/Alyoum

Kumekuwepo repoti za vyombo vya habari kwamba walikuwa wamejipatia makombora ya kudungulia ndege kwa kutumia mabega lakini makombora hayo yanaweza kufanya kazi kwa kudungulia ndege na helikopta zinazoruka umbali mdogo kutoka ardhini.Wanamgambo hao waliojikita Sinai hapo mwezi wa Januari walidai kuwa wameiangusha helikopta ya kijeshi ambapo serikali ya Misri ilikiri kuanguka kwa helikopta hiyo bila ya kutowa sababu.

Waziri wa usafiri wa anga Hossam Kamal amesema timu ya uchunguzi imewasili katika eneo la ajali kuyachunguza mabaki ya ndege hiyo na kutafuta visanduku vya rekodi ya safari.Nayo kamati ya uchunguzi ya Urusi ambacho ni chombo cha juu cha uchungiuzi nchini humo kwa mujibu wa msemaji wake Sergei Markin imeanzisha uchunguzi wa ajali hiyo.

Ilipoteza mawasiliano

Mapema Jumamosi afisa wa Misri wa kamati inayoshughulikia ajali za anga ameviambia vyombo vya habari kwamba ndege hiyo ilipoteza mawasiliano kwa muda lakini baadae ikawa iko kwenye anga ya Uturuki ikiwa salama.

Alexei Anikin (wa kwanza kushoto) mkuu wa Wizara ya masuala ya dharura akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Pulkovo mjini St. Petersburg.(31.10.2015).Picha: picture-alliance/dpa/A. Demianchuk

Baadae afisa huyo huyo Ayman al -Muqadem alisema ndege hiyo imeanguka na kwamba rubani wake kabla ya kupoteza mawasiliano alituma ujumbe wa radio kwamba ndege hiyo ilikuwa ikikabiliwa na matatizo ya kiufundi na kwamba alikuwa akijaribu kutuwa katika uwanja wa ndege ulio karibu.

Takriban watalii milioni tatu wa Urusi au theluji moja ya watalii wote waliotembelea Misri hapo mwaka 2014 wanakwenda Misri kila mwaka na wengi wao hutembelea miji ya kitalii ya Bahari ya Sham, Sinai au eneo la bara nchini Misri.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters/AFP

Mhariri : Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW