N'DJAMENA:Wahudumu wa ndege wa Uhispania na Ubelgiji waachiwa
9 Novemba 2007Mahakama nchini Chad imewaachia huru wahudumu watatu wa ndege wa Kihispania na rubani mmoja wa Ubelgiji waliokuwa wakizuiliwa kwa kuhusika na njama ya kuwateka zaidi ya watoto 100 wa Kiafrika na kuwasafirisha hadi barani Ulaya.
Watuhumiwa hao wanatarajiwa kurejea barani UIaya hii leo.Watu hao wane waliachiwa baada ya kushtakiwa kwa madai ya kuhusika na njama ya kuwateka watoto hao wa Kiafrika kupitia shirika la kutoa misaada kwa watoto Zoes Ark.
Wafanyikazi sita wa shirika hilo la Kifaransa wanashtakiwa kwa jaribio la kuwateka watoto na wanaendelea kuzuiliwa nchini Chad.Endapo watapatikana na hatia huenda wakahukumiwa kifungo cha miaka 20 kinachoambatana na kazi ngumu.Nchi ya Uhispania imepongeza hatua ya kuachiwa huru kwa raia wake.
Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa na nyingine zinashuku madai ya shirika hilo la msaada la Zoe’s Ark linaloshikilia kuwa watoto hao 103 ni yatima kutoka eneo la magharibi la Darfur nchini Sudan.Eneo hilo limezongwa na vita tangu mwaka 2003 vilivyosababisha maelfu kuyahama makazi yao na kutorokea nchi jirani ya Chad.Zaidi ya watu laki mbili wanaripotiwa kupoteza maisha yao katika mgogoro huo kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya kutoa misaada.