Ndoto ya Guendogan ya Euro 2016 yakatizwa
6 Mei 2016Klabu hiyo ya Bundesliga imesema Guendogan mwenye umri wa miaka 25, aliumia goti la wakati anafanya mazozi na atakuwa nje ya uwanja wka mechi mbili zilizosalia msimu huu, fainali ya Kombe la Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB Pokal dhidi ya Bayern Munich pamoja na Euro 2016.
Habari hizo ni pigo kwa kocha wa timu ya Ujerumani Joachim Loew na pia bahati mbaya mchezaji huyo aliyekosa Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil kutokana na maumivu ya mgongo yaliyomweka mkekani kwa miezi 14 kuanzia Agosti 2013.
Loew amekuwa na matatizo kadhaa ya majeruhi ambapo Bastian Schweinsteiger, Julian Draxler, Emre Can, Jerome Boateng na Benedikt Hoewedes wote wakiwa nje mwaka huu. Hata hivyo matatizo hayo yamepungua karibuni ambapo Can, Boateng na Hoewedes wamerejea, na kiungo wa Wolfsburg Draxler akianza tena mazoezi ya timu yake. Loew anatarajiwa kukitaja kikosi cha mwanzo cha Euro 2016 mnamo Mei 17. Ujerumani itacheza mechi yake ya kwanza ya dimba hilo litakaloandaliwa Ufaransa, Juni 12 dhidi ya Ukraine mjini Lille, na pia itachuana na Ireland ya Kaskazini na Poland katika Kundi C.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu