1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndovu barani Afrika waathirika na uwindaji haramu

25 Machi 2021

Ripoti iliyotolewa Alhamisi na shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira IUCN inasema kuwa ongezeko la tishio la uwindaji haramu na kuharibika kwa mazingira kumehatarisha idadi ya ndovu barani Afrika.

Afrika Steppe und Savanne Kenia
Picha: R. de Haas/AGAMI/blickwinkel/picture alliance

Ndovu wa misitu ya Afrika wanakabiliwa na hatari kubwa na wale wanaoishi katika maeneo ya vichaka na nyasi pia wanakabiliwa na hatari. Aina hizo mbili za ndovu awali zilikuwa zimejumuishwa kama aina moja na kuorodheshwa na shirika hilo la IUCN kama inayokabiliwa na hatari.

Kulingana na shirika la IUCN ambalo linakadiria athari za kuangamia kwa wanyama pori duniani, idadi ya ndovu wa misitu ya Afrika imepungua kwa zaidi ya asilimia 86 katika muda wa miaka 31 huku ile ya wale wanaoishi katika maeneo ya vichaka na nyasi ikipungua kwa asilimia 60 katika kipindi cha miaka 50.

Kwa mujibu wa shirika hilo, bara la Afrika kwa sasa lina ndovu 415,000 wakijumuishwa wa aina zote mbili.

Mahali wanapopatikana ndovu hao

Ndovu wanaoishi katika maeneo ya vichaka na nyasi wanapendelea nyanda za wazi zaidi na hupatikana katika

makazi tofauti katika eneo la Jangwa la Sahara, huko Botswana, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Ndovu wanaoishi katika misitu ya Afrika ambao ni wachache, wengi huishi katika misitu ya maeneo ya tropiki katika eneo la Magharibi na Kati mwa Afrika huku idadi kubwa iliyosalia ikipatikana nchini Gabon na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Ndovu katika jangwa la SaharaPicha: Zoonar.com/David Freigner/picture alliance

Waziri wa maji na misitu nchini Gabon, Lee White, ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa vita dhidi ya uwindaji haramu wa ndovu ni zaidi ya kupigania mazingira na kwamba ni kupigania uthabiti wa taifa hilo. White amesema wameshuhudia mataifa kama Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo wawawindaji haramu hugeuka kuwa majambazi, waasi na kudhoofisha taifa zima na kusema uwindaji haramu wa kiwango cha juu na uuzaji wa pembe za ndovu unatokana na makundi ya kimataifa yanayoendeleza biashara hiyo.

Tatizo lingine linalochangia kuangamia kwa ndovu hao

Rudi Van Aarde wa chuo kikuu cha idara ya elimu ya wanyama ya Pretoria amesema makundi ya uhalifu yanayoshirikiana na maafisa fisadi pia ni tatizo kubwa katika eneo la Kati na magharibi mwa Afrika. Rudi anasema pembe nyingi za ndovu zinazotolewa barani na kupelekwa barani Asia ni kutoka Afrika ya Kati na Magharibi. Idadi hiyo inaathirika zaidi kwa sababu ya biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu badala ya masuala ya mazingira kama vile ukataji miti.

Ndovu wanaoishi katika maeneo ya vichaka na nyasi waliathirika vibaya kutokana na ongezeko la uwindaji haramu kati ya mwaka 2008 na 2012. Aarde anasema mtindo unaotia hofu ni kwamba kiwango kikubwa cha uwindaji haramu kilitokea katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika ambapo makadirio ya ndovu 100,000 wanaoishi katika maeneo ya vichaka na nyasi waliuawa katika eneo la Kaskazini mwa Msumbiji na Kusini mwa Tanzania wakati wa kipindi hicho.