1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndowa ya watu wa jinsia moja huenda ikaruhusiwa Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
28 Juni 2017

Mada iliyohanikiza magazetini hii leo inahusu "ndoa ya mashoga", uwezekano wa kupitishwa sheria hivi karibuni inayoruhusu watu wa jinsia moja kuoana nchini Ujerumani naa kuapishwa Armin Laschet kuwa waziri mkuu NRW

Symbolbild Homo-Ehe
Picha: picture-alliance/dpa

 

Tunaanzia na habari zilizogonga vichwa vya habari baada ya kansela Angela Merkel kutamka katika mahojiano na jarida la Brigitte, haoni pingamizi kama watu wa jinsia moja wataoana. Kwa namna hiyo kansela Merkel amemaliza udhia. Na bunge la shirikisho linatarajiwa kuidhinisha mswaada wa sheria kuhusu ndoa ya mashoga wakati wowote kutoka sasa. Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika: "SPD wamewabana wana CDU/CSU kwa namna ambayo Angela Merkel hakuwa na njia nyengine isipokuwa kufanya kile alichobidi kukifanya: Ameligeuza suala la kupigiwa kura ndoa ya mashoga kuwa ni la nafsi ya mtu na kwa namna hiyo kulifungulia milango. Hakuna tena kushurutishwa makundi ya wawakilishi bungeni. Baadhi ya wenzake chamani wamekasirishwa kupita kiasi na ridhaa ya kulazimishwa. Na kwa Merkel pia hakuna uhakika."

 

Gazeti la "Berliner Morgenpost" linajiuliza kama SPD na vyama vya upinzani havijandaa njama dhidi ya vyama ndugu vya CDU/CSU. Gazeti linandelea kuandika: "Mara nyingi kampeni za uchaguzi zinakuwa zinachosha hasa wanapozungumzia mambo yale yale, kodi za mapato, elimu, na fursa sawa. Katika majadiliano ya kuunda serikali za muungano ahadi zinazotolewa tokea hapo hazitekelezwi. Ndio maana ni jambo la kusisimua kuona jinsi mvutano wa miaka kadhaa, yaani ndoa ya mashoga, kufumba na kufumbua unapatiwa sura ya kisiasa. Matokeo yake hayajulikani, washindi na watakaoshindwa pia hawajulikani. Je, Kansela na kupenda kwake kubadilisha msimamo bila ya kutarajiwa atashinda? Au SPD pamoja na vyama vya upinzani wameandaa njama kusababisha mfarakano ndani ya vyama ndugu vya CDU/CSU?"

 

North Rhine Wesphalia yajipatia waziri mkuu mpya

 

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linahisi uamuzi wa kansela Merkel ni wa maana hata kama unawaudhi baadhi ya wanachama wa CDU/CSU. Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha mjini Düsseldorf alikoapishwa jana waziri mkuu wa serikali ya jimbo la North Rhine Westphalia. Gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger linaandika: "Armin Lachet anabidi sasa atekeleze kile alichoahidi kama anataka kweli jimbo la North Rhine Westphalia NRW ligeuke mhimili wa serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na FDP uchaguzi mkuu utakapoitiswa miezi mitatu kutoka sasa. Wakaazi wengi wa eneo hili la mto Rhine wanamwekea matumaini yao waziri mkuu huyo anayetokea katika eneo la Aachen. Hata kama anakotokea mwanasiasa si muhimu lakini pindi Laschet akifanikiwa kupigania vyema zaidi masilahi ya jimbo hili mjini Berlin, basi eneo lote la mto Rhine ndilo litakalofaidika.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW