Virusi Trojaner vyavuruga data za bunge la shirikisho
11 Juni 2015Tunaanzia lakini na mjadala kuhusu ndowa ya watu wa jinsia moja na jinsi unavyoutia sumu uhusiano kati ya washirika wa serikali ya jimbo mjini Berlin.Gazeti la "Berliner Morgenpost" linaandika:"SPD na CDU wametumbukia katika bahari ya mizozo kwasababu ya ndowa ya watu wa jinsia moja itakayojadiliwa kesho na baraza la wawakilishi wa majimbo-Bundesrat mjini Berlin.Kwasababu chama cha Social Democratic na diwani wake mjini Berlin Michael Müller wanatia kishindo sheria ya ndowa ya watu wa jinsia moja itumike pia nchini Ujerumani.Ni mada ya kusisimua inayoweza kuwavutia wapiga kura na hasa miongoni mwa mashoga mjini Berlin.Ni mada tete lakini kwa CDU-kwasababu chama kikuu cha Christian Democratic kinapinga moja kwa moja ndowa ya aina hiyo.Pindi Müller akithubutu kweli kunyanyua mkono hapo kesho,basi Henkel ataivunja serikali ya muungano mjini Berlin seuze tena amepania kuona mkutano mkuu wa chama katika jimbo la Berlin unamchagua tena kuwa mwenyekiti wao siku ya pili yake .Atashindwa kuwatanabahisha wajumbe wa chama chake kwanini anakubali kuendeshwa mbio na Müller.
Udukuzi katika bunge la shirikisho
Kisa cha udukuzi kimeliathiri bunge la shirikisho -Bundestag mjini Berlin. Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika:"Mpaka bunge la shirikisho haliko salama.Virusi vya mtandao kwa jina "Trojaner" vimevuruga data zote.Kwa upande mmoja mtu anaweza kuchekelea kuona kwamba uharibifu kama huo umeathiri mpaka taasisi yenye kujivunia ulinzi wa hali ya juu humu nchini.Lakini ukiangalia kwa makini,unashindwa kucheka.Kwasababu unajiambia taasisi kama hiyo hasa ndiyo inayobidi kulindwa ipasavyo dhidi ya hujuma kutoka nje.Lakini ndio kwanza tunasikia kisa hiki si cha leo,kimeanza tangu wiki nne zilizopita.Pengine kansela Angela Merkel awaulize watumishi wa shirika la upelelezi la Marekani NSA kuhusu nini la kufanya katika kadhia kama hii.Au pengine ana wasi wasi isiwe hujuma hizo zinatokea huko huko.Hakuna ajuaye kwa uhakika."
Wananchi wa jumuia ya NATO wanapenda amani
Na hatimaye tuiangalie kura ya maoni ya wananchi wa jumuia ya kujihami ya NATO kuhusu suala kama jumuia hiyo iipatie silaha Ukraine au la.Gazeti la "Badisches Tagblatt" linaandika:"Pengine kura ya maoni kama hiyo inayofanyika kwa wakati maalum tu,haistahiki kupewa umuhimu.Hata hivyo matokeo yake yanastaajabisha kwa kila hali:Kiu cha kutaka amani kimeenea kila pembe na pengine wasi wasi wa wakaazi wa nchi za magharibi si wa bure ukitiliwa maanani msimamo wa NATO katika mzozo wa Ukraine.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Josephat Charo