1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEC yakataa mapingamizi ya Lissu dhidi ya Magufuli, Lipumba

George Njogopa27 Agosti 2020

Tume ya Uchaguzi Tanzania NEC imetupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na mgombea wa CHADEMA, Tundu Lissu dhidi ya mgombea wa chama tawala CCM, Rais John Magufuli pamoja na mgombea wa chama cha CUF, Profesa Lipumba.

Leiter der Wahlkommission NEC in Tansania
Picha: DW/S. Khamis

Uamuzi wa tume hiyo unamaanisha kwamba idadi ya wagombea wa urais katika kinyang'anyiro hicho inaendelea kusalia 15, kama walivyoteuliwa na tume hiyo hapo Oktoba 25.

Tume hiyo imesema sababu zilizowasilishwa na mgombea Lissu aliyetaka wagombea hao wawili waenguliwe kwenye mbio hizo zilikuwa hazina uzito wowote.

Miongoni mwa sababu zilizotolewa na Lissu katika mapingamizi yake ni pamoja na mgombea wa CCM kuwasilisha picha ambazo haziendani na maelekezo yaliyopo kwenye kanuni za uchaguzi.

Hoja nyingine ni ile inayosema kwamba wagombea hao wawili Rais Magufuli na Profesa Lipumba kuhakiki majina ya wadhamini kupitia wasimamizi wa uchaguzi majimboni jambo ambalo alidai ni kinyume na maelekezo yaliyomo kwenye sheria za uchaguzi.

Rais Mgufuli na mgombea mwenzake Samia Hassan Suluhu.Picha: DW/S. Khamis

Akisoma uamuzi wa tume baada ya kupitia mapingamizi hayo, mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo, Dk Wilsoni Mahera amesema, wagombea wote wawili hakuna pahala walipokiuka sheria hizo.

Hadi jana jioni ambayo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa wagombea wanaokusudia kuweka pingamizi kujitokeza ni wagombea hao wawili tu ndiyo waliokumbana na pingamizi hilo.

Kwa maana hiyo sasa tume imefungua milango kwa wagombea wote 15 waliopitishwa kuendelea na mchakamchaka wa kampeni.

Mapingamizi dhidi ya wagombea ubungu, udiwani

Ingawa tume hiyo imemaliza kutegua kitendawili cha wagombea wa nafasi ya urais, bado kumekuwa na idadi kubwa ya mapingamizi kutoka kwa wagombea wengine wa ubunge na udiwani, jambo ambalo linatajwa kwamba ni la kwanza kushuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa na idadi kubwa ya mapingamizi.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika wagombea wake kuenguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho katika mazingira ya kutatanisha hatua iliyovifanya kupiga hodi katika ofisi za tume hiyo kusaka ufumbuzi.

Mgombea urais wa chama cha CUF profesa Ibrahim Lipumba na mgombea mwenza wake Hamida Abdallah Huaeshi walipokabdhiwa fomu ze uteuzi na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage (kulia) Agosti 10, 2020.Picha: DW/S. Khamis

Na wakati huu kukiwa bado haijafahamika hatma ya wagombea wengi, kunashuhudiwa hamasa ndogo ya kampeni na huenda hali hiyo ikaanza kubadilika mwishoni mwa wiki.

Chama tawala CCM, kimepanga kuzindua kampeni zake tarehe 29 jijini Dodoma siku ambayo pia itaainisha sera zake kuelekea katika uchaguzi huo.

Chama cha ACT Wazalendo kilisemekana kuwa na mpango wa kuanzisha kampeni zake tarehe kama hiyo yaani 29 huko Lindi lakini baadhi ya duru za habari zinasema kwamba huenda tarehe na eneo la kuanzisha kampeni likabadilishwa.

Chama kikuu cha upinzani hakijkasema lolote ni lini kitaanzisha kampeni zake ingawa kuna uwezekano mkubwa wa shughuli hiyo itaanzia katika jiji la Dar es salaam.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW