1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu akutwa na hatia ya kukiuka maadili ya uchaguzi

Hawa Bihoga2 Oktoba 2020

Mgombea Urais kupitia Chadema Tundu Lissu amesema hakubaliani na maamuzi ya tume ya taifa ya uchaguzi ya kumsimamisha siku saba kufanya kampeni baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka maadili ya uchaguzi.

Tansania Dar es Salaam | Politiker | Tundu Lissu
Mgombea wa Urais kupitia Chadema Tundu LissuPicha: DW/S. Khamis

Tundu Lisu amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Dar es salaam, ikiwa ni muda mfupi baada ya kusambaa kwa taarifa za kusimamishwa kwa mgombea huyo kufanya kampeni kwa siku saba baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka maadili ya uchaguzi.

Mgombea huyo wa chama cha CHADEMA ambaye ameonenakana kufedheheshwa na uamuzi huo amesema hakuna malalamiko yoyote ambayo yamemfikia kuwa amekiuka maadili yalioanishwa na tume kwenye barua ya kumsimamisha, hivyo ameutafsiri uamuzi huo kuwa si wa haki kwa kuwa haukufata utaratibu wa sheria na hivyo ataendelea na kampeni za uchaguzi kama ilivyo kwenye ratiba ya kampeni za uchaguzi.

Lissu  amesema: "Wakati kamati kuu  tunasubiri tuweke msimamo wa chama, msimamo wangu binafsi ni kwamba kampeini zitaendelea siku ya Jumapili kama ambavyo imepnagwa kwenye ratiba iliyoratibiwa na tume ya uchaguzi. Kwa hio msimamo ndio huo.Mimi najiandaa kwa mikutano ya kampeni siku ya Jumapili".

Lissu amesema wamewasilisha malalamiko kwa NEC

Tanzania itaanda uchaguzi mkuu Oktoba 28Picha: DW/S. Khamis

Aidha Lissu amesema tayari wamewasilisha malalamiko kadhaa kwa tume ya taifa ya uchaguzi wakimtuhumu mgombea wa chama tawala CCM Rais John Pombe Magufuli kukiuka maadili ya uchaguzi lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, hivyo ameitafsiri tume ya uchaguzi kuwa haipo huru katika kutekeleza majukumu yake.

Tume ya taifa ya uchaguzi kupitia mkurugenzi wake wa huduma za sheria Emnuel Kavishe ambaye ndio amesaini waraka wa kumsimamisha Lissu kufanya kampeni zake kwa siku saba, amesema mgombea huyo anayo nafasi ya kukata rufaa katika maamuzi hayo.

Awali leo hii kabla ya uamuzi wa kumsimamisha, jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es slaam lilitengua barua yake ya kumuita kwa ajili ya mahojiano na kumruhusu kuendelea na shughuli zake za kampeni, kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa amewaambia wanahabari.

Wakati hayo yakiendelea msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania jaji Fransis Mutungi amefanya mkutano na viongozi wa vyama vya siasa na kuwasihi kufanya kampeni za kiistarabu na zinazoheshimu sheria ili kumaliza zoezi hilo la kidemokrasia kwa amani na utulivu.

 

Mwandishi: Hawa Bihoga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW