1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Nelson Chamisa, kijana anayepambana na Mnangagwa

23 Agosti 2023

Mwanasiasa mzoefu aliye na miongo kadhaa ya uanaharakati ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa wa umri wa miaka 45, bado anajulikana na wengi kama "mukomana au "kijana".

Mgombea wa upinzani Chamisa
Nelson Chamisa wa chama cha CCCPicha: KB MPOFU/REUTERS

Jina hilo la utani linaonesha pengo la umri kati ya mgombea huyo wa urais na mpinzani wake mkuu katika kura ya Agosti 23, rais wa sasa Emmerson Mnangagwa, wa umri wa miaka 80. Pia linatumika kuepuka kutaja jina la mwanasiasa huyo hadharani katika taifa ambalo makundi ya haki yanasema rais huyo ameanzisha msako mkali dhidi ya wapinzani. 

Mzaliwa wa Masvingo, kusini mwa mji mkuu Harare, Chamisa alisomea sheria na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe na pia ana shahada ya theolojia.

Chamisa anasema mafaniko yake ya kitaaluma yanatokana na msisitizo wa wazazi wake kwamba anapaswa kuthamini elimu na kufaulu shuleni. Kama mkuu wa muungano wa kitaifa wa wanafunzi nchini Zimbabwe, mwishoni mwa miaka ya 1990, Chamisa alikuwa miongoni mwa waandaaji wa maandamano dhidi ya serikali ya Mugabe ambayo yalisababisha vyuo vikuu kufungwa. Chamisa ameoa na ana mtoto mmoja.Zimbabwe yashutumiwa kukiuka taratibu kabla ya uchaguzi

Umati wa wafuasi wa ChamisaPicha: KB MPOFU/REUTERS

Alijiunga na chama pinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kama mwanafunzi wakati kilipoundwa mnamo mwaka 1999 na kuanza kukiongoza baada ya kifo cha mkufunzi wake na kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai, mnamo mwaka 2018.

Mwaka huo huo Chamisa alikaribia kumshinda Mnangagwa katika uchaguzi mkali, wa kwanza kufanyika baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe. Alipinga matokeo mahakamani lakini akashindwa.

Mwaka jana, Chamisa alikihama chama cha MDC na kuunda chama cha CCC, chama cha pekee kilicho na matumaini ya kukiondoa madarakani chama tawala cha ZANU-PF, ambacho kimekuwa uongozini tangu uhuru mnamo mwaka 1980. Lakini bado kinakabiliwa na changamoto nyingi.

Chamisa ameahidi kuunda Zimbabwe mpya kwa kila mmoja, kukabiliana na ufisadi, kufufua upya uchumi na kuiondoa nchi hiyo katika hali ya kutengwa kimataifa.

Wapiga kura wengi waliochukizwa na umaskini ulioenea na mfumuko wa bei wanamuunga mkono, lakini hajaepuka ukosoaji hata kutoka ndani ya chama chake mwenyewe. Nicole Beardsworth, mchambuzi wa kisiasa na mtaalamu kuhusu Zimbabwe katika chuo kikuu cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini anasema mtindo wa uongozi wa Chamisa wa kuthibiti kila kitu umedhoofisha mifumo ya chama chake.

Chamisa wakati wa kampeniPicha: KB MPOFU/REUTERS

Uchaguzi wa Agosti 23: Zimbabwe yatangaza Agosti 23 kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu

Hii inatokana na hofu kuwa kinaweza kuingiliwa na chama tawala. Lakini wakosoaji wanasema mfumo huo , umekidhoofisha chama cha CCC, na kusababisha mkanganyiko na ukosefu wa mpangilio katika maandalizi ya uchaguzi. Baadhi wanalalamika kuwa Chamisa hajachukuwa hatua za kutosha katika kutafuta uhuru wa afisa mkuu na mbunge maarufu wa chama cha CCC Job Sikhala, ambaye amekaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja na pia ameshindwa kueleza maono mbadala kwa Zimbabwe.

Uchambuzi kuhusu maandalizi ya uchaguzi: 

Hali ya siasa nchini Zimbabwe kuelekea uchaguzi

This browser does not support the audio element.

Baadhi ya mikutano ya hadhara imezuiwa, baadhi ya wanachama wake kukamatwa na kutupwa gerezani na hofu ya kuibiwa kura imetanda. Chamisa ameshuhudia yote.  Chamisa amekamatwa mara kadhaa kwa shughuli zake za kisiasa. Mnamo 2007, alipigwa kwa viboko vikali na chuma na kuachwa kufa. Alikaa siku tano hospitalini baada ya shambulio hilo, ambalo lilihusishwa pakubwa na majambazi wa chama tawala.

Dini ni mada ya hivi sasa katika ujumbe wa Chamisa, lakini wachambuzi wanasema imetenga baadhi ya maeneo ya mjini ambapo chama hicho kina ufuasi mkubwa. Neno Mungu limejitokeza mara 40 katika manifesto ya CCC ambayo inajumuisha miongoni mwa masuala ya kipaombele , kuifanya Zimbabwe kuwa taifa linalompenda na kumuogopa Mungu. Kauli mbiu ya kampeini ni "Mungu yuko ndani yake''.

 

     

  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW