1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aahidi 'nguvu, dhamira' dhidi ya Wahuthi Yemen

22 Desemba 2024

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ameapa kulipiza kisasi dhidi ya Wahuthi nchini Yemen baada ya kuishambulia Tel Aviv, akisema Israel itashambulia kile alichokiita mkono wa mwisho wa "mhimili wa uovu wa Iran."

Maeneo ya Wapalestina | Netanyahu na makamanda wake
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin ( wa pili kulia), Netanyahu akishauriana na viongozi wa jeshi.Picha: Maayan Toaf/Israel Gpo/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu Jumapili aliahidi kulipiza kisasi dhidi ya waasi wa Huthi wa Yemen baada ya kurusha kombora kuelekea Tel Aviv, akionya kwamba Israel itashambulia kile alichokiita mkono wa mwisho uliosalia wa "mhimili wa uovu wa Iran."

Wahuthi walikishambulia kitovu cha kibiashara cha Israel Jumamosi kwa kile walichodai kuwa kombora la masafa marefu, na kuwajeruhi watu 16 huku wengi wakilazimika kuyahama makazi yao kufuatia shambulio hilo lililofanyika kabla ya alfajiri.

"Vile tulivyoshughulika kwa nguvu dhidi ya mikono ya kigaidi ya mhimili wa uovu wa Iran, ndivyo tutakavyoshughulika dhidi ya Wahuthi.. kwa nguvu, dhamira na ujanja," alisema Netanyahu katika taarifa ya video.

Shambulio la Jumamosi mjini Tel Aviv lilikuwa la pili la aina hiyo dhidi ya Israel kutoka kwa Wahuthi wiki hii, na mojawapo ya mashambulio mengi tangu vita vya Gaza vilipoanza.

Eneo lilikoanguka kombora la Wahuthi mjini Tel AvivPicha: Itai Ron/REUTERS

Wahuthi wanaoungwa mkono na Iran wanasema wanafanya mashambulizi kwa mshikamano na Wapalestina katika vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Vita hivyo vilianza Oktoba 7, 2023, kufuatia shambulio lililofanywa na Hamas dhidi ya Israel.

Soma pia: Netanyahu atoa oanyo kali kwa Wahouthi wa Yemen

Kauli ya hivi karibuni ya Netanyahu ilikuja baada ya Marekani kusema kwamba ilishambulia maeneo katika mji mkuu wa Yemen unaoshikiliwa na waasi, Sanaa, Jumamosi, saa chache baada ya Wahuthi kuishambulia Tel Aviv.

Miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa ilikuwa kituo cha kuhifadhi makombora cha Wahuthi na "kituo cha kamandi na udhibiti," kulingana na taarifa ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM).

Vikosi vya Marekani pia vilidungua droni kadhaa za Wahuthi na kombora moja la masafa marefu juu ya Bahari ya Shamu, ilisema.

Meli ya Marekani yadungua ndege yao kwa bahari mbaya

Hata hivyo, marubani wawili wa Jeshi la Wanamaji la Marekani walidunguliwa juu ya Bahari ya Shamu mapema Jumapili katika "tukio la wazi la shambulio la bahati mbaya," lilisema jeshi la Marekani.

Wahuthi baadaye walidai "kuilenga" meli ya kubeba ndege ya USS Harry S Truman siku moja kabla katika operesheni iliyosababisha "kudunguliwa kwa ndege moja ya F-18."

Marekani na vikosi vya Uingereza vimekuwa vikishambulia mara kwa mara maeneo ya waasi huko Yemen kujibu mashambulio ya Wahuthi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, ambayo ni muhimu kwa biashara ya kimataifa.

Israel pia imewahi kuwashambulia Wahuthi, ikilenga bandari na miundombinu ya nishati, baada ya mashambulio ya waasi dhidi ya ardhi yake.

Marekani na Uingereza zimekuwa zikifanya mashambulizi dhidi ya Wahuthi lakini mashambulizi hayo hayajawazuwia.Picha: CENTCOM/Handout/Anadolu/picture alliance

Shambulio la hivi karibuni la Israeli dhidi ya Wahuthi lilikuwa siku ya Alhamisi, ambapo ndege za kivita za Israeli ziliushambulia mji wa Sanaa kwa mara ya kwanza.

Soma pia: Israel yashambulia miundombinu ya Wahouthi Yemen

Majibu ya Israeli yalikuja mara baada ya waasi kufyatua kombora lililoharibu shule moja nchini Israeli.

Jumapili, Netanyahu alikiri msaada wa Marekani, akisema kuwa Israel "haiko peke yake" katika mapambano yake dhidi ya Huthis.

"Marekani, pamoja na nchi nyingine, zinawaona Wahuthi kama tishio sio tu kwa usafirishaji wa kimataifa - bali kwa mpangilio wa kimataifa," alisema Netanyahu katika taarifa yake ya video.

Mkono mwa mwisho wa "mimili wa uovu" wa Iran

Katika taarifa nyingine iliyotolewa mapema wiki hii, Netanyahu alisema Wahuthi wangelipa "gharama kubwa sana" kwa mashambulio yao dhidi ya Israel.

"Baada ya Hamas, Hezbollah na utawala wa (Bashar al-)Assad huko Syria, Wahuthi ndiyo mkono wa mwisho wa mhimili wa uovu wa Iran," alisema.

"Wanagundua, na watagundua kwa njia ngumu kwamba yeyote anayeihujumu Israel - atalipa gharama kubwa sana."

Mbali na Hamas, Israel imepambana na makundi yanayoungwa mkono na Iran kote katika ukanda huo tangu vita vya Gaza vilipoanza, wakiwemo Wahuthi na vita kamili dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon.

Soma pia: Marekani yashambulia ngome 15 za Wahouthi, Yemen

Kampeni hizo zimewaua viongozi kadhaa wa Hamas na Hezbollah, wakiwemo mpangaji mkuu wa shambulio la Oktoba 7, kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, pamoja na makamanda wa Iran.

Wahouthi wasema wamemuua Ali Abdallah Saleh

02:20

This browser does not support the video element.

Israel pia ilimuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah, huku mtangulizi wa Sinwar, Ismail Haniyeh, akiuawa katika shambulio la kijasiri mjini Tehran, ambalo Iran na Hamas wameilaumu Israel.

Israel pia iliishangaza Hezbollah kwa mashambulio yaliyohusisha kuripua vifaa vya mawasiliano na redio yaliowaua makumi ya wapiganaji wake na kuwajeruhi maelfu, kulingana na mamlaka za Lebanon.

Mwisho wa Novemba, Israel na Hezbollah walikubaliana kusitisha mapigano, ambayo yamesitisha kampeni kali ya mabomu ya Israel ndani ya Lebanon lakini wanajeshi wa Israeli bado wanaendelea kuwepo kusini mwa nchi ghiyo jirani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW