Netanyahu aapa kuiunganisha Israel
24 Machi 2023Haya yanakuja wakati upinzani dhidi ya mageuzi hayo ukiongezeka na ukizuwa wasiwasi wa mpasuko kwenye taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Kwenye hotuba kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Netanyahu amesema anatambua wasiwasi wa pande zote, ingawa hakuelezea kwa kina ni kwa namna gani ataushughulikia mpasuko huo.
Hotuba ya usiku wa jana ya Netanyahu imekuja baada ya siku nyingine ya maandamano makubwa kote nchini humo ya kuupinga mpango wake huo, na masaa kadhaa baada ya muungano wake kwenye bunge kupitisha sheria ya kwanza miongoni mwa msururu wa sheria zinazopelekea mageuzi hayo.
Netanyahu amesema: "Namna bora ya kufikia mageuzi yenye uwiano na kuzuia mpasuko katika taifa ni kupitia mashauriano na kufikia maafikiano mapana zaidi. Ninapigania kufikia suluhu, ninafuatilia kwa umakini mashaka ya upande mwingine.
Soma pia: Israel imepitisha sheria itakayomlinda Netanyahu
Netanyahu amesema anatambua wasiwasi wa pande zote na hasa wa wapinzani wake, huku akiitupia lawama Mahakama ya Juu kwa kuingilia masuala ya kisiasa na kuongeza kuwa atahakikisha kila raia anapata haki zote za msingi, awe Myahudi ama asiye Myahudi, mwenye dini na mpagani, wanawake na hata jamii ya wapenzi wa jinsia moja. Amesisitiza kwamba atafanya kila liwezekanalo kurejesha utulivu.
Hata hivyo, ametoa hotuba yake wakati huko mitaani kote nchini Israel, maelfu ya raia wakiendelea kuandamana, ikiwa ni pamoja na kundi kubwa lililokusanyika nje ya makaazi yake binafsi yaliyoko mjini Jerusalem.
Ilimlazimu hata kusogeza mbele muda wa kuondoka kwenda nchini Uingereza kwa ziara rasmi ya kikazi hadi saa 10 za alfajiri hii leo ili kukabiliana kwanza na mzozo nchini mwake.
Upinzani watoa wito wa kuupinga mpango wa Netanyahu
Waandamanaji walizuia barabara kuu na kukabiliana vikali na polisi na hakukuwa na dalili yoyote kwamba makabiliano hayo yangetulizwa. Iliwalazimu polisi kutumia mabomba ya maji kuwatawanya waandamanaji na wengi miongoni mwao, ikiwa ni pamoja na viongozi wa vuguvugu hilo la waandamanaji, walikamatwa.
Aidha, vuguvugu hilo la waandamanaji liliyapinga mara moja matamshi hayo ya Nretanyahu, likisema wataendelea kupinga jaribio lake la kuwa dikteta. Kiongozi wa upinzani, Yair Lapid, amesema Netanyahu ameweka dhahiri kwamba hana mpango wa kufanya mazungumzo ya kweli na kuwatolea mwito wanachama wanaojitambua wa chama cha Likud cha Netanyahu kuupinga mpango huo.
Soma pia: Maandamano yaendelea Israel, huku Netanyahu akifanya ziara Ujerumani
Netanyahu na washirika wake wanataka kudhoofisha mamlaka ya mahakama, wakisema majaji wa mahakama ya juu zaidi ambao hawachaguliwi pamoja na majaji wengine wanajichukulia madaraka ya juu mno.
Wakosoaji wanasema mabadiliko hayo ambayo yatampatia Netanyahu na washirika wake wa kihafidhina mamlaka ya mwisho katika kuwachagua majaji, yataharibu kabisa utoaji wa haki katika mfumo wa mahakama na wanamshutumu Netanyahu kuwa na mgongano wa kimaslahi kwa kuwa anakabiliwa na kesi za kadhaa za ufisadi.
Mpango huo wa serikali umeliingiza taifa hilo lenye karibu miaka 75 kwenye mizozo mibaya kabisa ya ndani kuwahi kushuhudiwa.