Netanyahu ahutubia UNGA, ayashutumu mataifa ya magharibi
26 Septemba 2025
Kabla Waziri huyo Mkuu kuanza kutoa hotuba, idadi kubwa ya washiriki walitoka nje. Wakati kiongozi huyo wa Israel akizungumza, kulisikika kelele karibu na eneo la ukumbi. Ujumbe wa Marekani, unaomuunga mkono Netanyahu katika kampeni yake dhidi ya Hamas ulikuwa umetulia tuli. Na kwa upande mwingine kulisikika makofi mara tu alipoanza kuhutubia.
Mataifa machache makubwa yaliyohudhuria kama Marekani na Uingereza hayakupeleka maafisa wake waandamizi ama mabalozi wao wakati wa hotuba hii na badala yake viti vyao vilijaa maafisa na wanadiplomasia wa ngazi za chini.
Netanyahu akasema hivi na hapa namnukuu, "viongozi wa magharibi wanaweza kukubaliana na mashinikizo, lakini ninawahakikishia kitu kimoja, Israel kamwe haitabadilika."
Ametumia jukwaa hilo kuyakosoa vikali mataifa ya magharibi kwa kulikumbatia suala la utaifa wa Palestina na kuyatuhumu kwa kubadilika ghafla kufuatia mashinikizo kutoka kwa wanaharakati na wengine wanaoishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
"Mataifa ya Magharibi ni kigeugeu"
Mbele ya hadhara hiyo Netanyahu pia hakusita kuzikosoa vikali hatua za mfululizo za kidiplomasia zilizochukuliwa na washirika wakuu wa Marekani, ambazo zimeongeza kutengwa kwa Israel kimataifa kutokana na jinsi inavyoendesha vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza, vita ambavyo sasa vina karibu miaka miwili.
Ameangazia hatua zilizochukuliwa na viongozi wa Ufaransa Uingereza, australia, Canada na mataifa mengine ya kulitambua Taifa la Palestina na kusema wamefanya hivyo licha ya unyama uliofanywa na Hamas Oktoba 7, 2023 ambao ulisifiwa sana na karibu asilimia 90 ya watu wa Palestina.
"Unajua viongozi waliolitambua taifa la Palestina wiki hii walituma ujumbe gani kwa Wapalestina... ni ujumbe wa wazi kabisa.. kwamba ni sawa kuwaua Wayahudi..." alisema Netanyahu.
Huku mataifa mengi zaidi yakijiunga kwenye orodha ya wanaoitambua rasmi Palestina kama dola huru, serikali ya mrengo wa kulia ya Israel imetoa tamko kali kabisa kwamba hakutawahi kuwepo Taifa la Palestina huku ikiendeleza vita dhidi ya Hamas. Hadi sasa Israel imewaua Wapalestina zaidi ya 65,000 wa Gaza hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa afya wa Gaza, huku eneo hilo zima likiwa limegeuzwa kuwa magofu.
ICC inamsaka Netanyahu kwa uhalifu wa kivita
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - ICC tayari imetoa waranti wa kukamatwa Netenyahu kwa madai ya uhalifu wa kivita huko Gaza. Israel lakini inapinga mamlaka ya mahakama hiyo na yeye mwenyewe anakanusha kufanya uhalifu wa kivita. Na hii leo alikosoa kile alichokiita "mashitaka ya uongo ya mauaji ya kimbari."
Hamas imejitolea kuwaachilia mateka wote waliosalia karibia 20, kati ya 48 wanaosemekana kuwa wangali hai, ili badala yake Israel ivimalize vita na kuondoka Gaza.